Thursday, 30 July 2015

Lissu wanaotaka kuondoka Chadema ruksa

MBUNGE wa Singida Mashariki na Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tundu Lissu, amesema chama chao kinatarajia kupata wanachama wengi baada Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa kujiunga na chama hicho.


Akizungumza leo na waandishi wa habari Lissu amesema, “Kama wapo watakao jiondoa Chadema, wengi zaidi watakuja. Tupo katika kipindi ambacho hatujawahi kuwepo tangu mfumo wa vyama vingi uanze. Mfumo tawala unabomoka vipande vipande. Unapo bomoka, dalili zake ni watu ambao wamekuwa katika mfumo huo kuondoka kama alivyofanya Lowassa.”

“Mabadiliko katika nchi yanatokea pale mfumo tawala unapo pasuka. Lowassa ni mfano mzuri. Tunamkaribisha kwetu sio kwa sababu ni mwanasiasa msafi. Tumempokea kwa sababu tunaongeza nguvu kubwa kwa wale wanaotaka mabadiliko. Imetokea Zambia Mawawi, Nigeria na Kenya,” amesema Lissu.

Akizungumza kuhusu Chadema kumtuhumu Lowassa kwamba “ni fisadi” kabla ya kujiunga na chama hicho Lissu amesema, “…hatukuwa na makosa hata kido kumweka Lowassa katika kundi la watuhumiwa wa Richmond. Mambo yalizungumzwa bungeni. Aliwajibika na amesema mwenyewe aliwajibika.”

“Alijiuzuru uwaziri mkuu kwa sababu ya Richmond. Tulimweka katika orodha ya mafisadi kwa sababu ya Richmond. Na jana alisema alimwambia rais “tuvunje mkataba” rais akaataa. Angefanyeje?. hilo ni vumbi, litakapo tulia Chama Cha Mapinduzi na mfumo tawala utakuwa umeanguka, tutajenga nchini.Bila kuvunja mfumo tawala hakuna kusonga mbele,” ameeleza Lissu.

Friday, 24 July 2015

TASWIRA: MAPOKEZI YA ESTHER BULAYA NA JAMES LEMBELI BUNDA.


Msafara wa bodaboda uliowapokea Mh Esther Bulaya na Mh James Lembeli walipofika Bunda kwa ajili ya kuhutubia mkutano mkubwa Jimboni Bunda.
Mh Esther Bulaya akisalimiana na Viongozi wa Chadema Bunda waliokuja kuwapokea.
Mbunge wa Viti Maalumu wa CCM aliyehamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Ester Bulaya akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Stendi ya zamani Mjini Bunda mkoani Mara.
Mbunge wa Kahama mkoani Shinyanga, James Lembeli aliyehama kutoka CCM na kujiunga Chadema, akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Stendi ya zamani ya mabasi Mjini Bunda jana
Umati wa wananchi wa Mji wa Bunda na viunga vyake, wakiwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Stendi ya zamani ya mabasi mjini Bunda jana, uliohutubiwa pia na Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya na mwenzake wa Kahama, James Lembeli waliotoka CCM na kuhamia Chadema.





Thursday, 23 July 2015

MATOKEO YA KURA YA MAONI UBUNGE YA CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)

Inaendelea..............

Mbowe: Watanzania Mtuvumilie


Mwanza/Dar. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema chama chake kimeshindwa kumtangaza mgombea wake wa urais kama ilivyotarajiwa jana, badala yake kikawaomba Watanzania kutokuwa na haraka, wasiwasi wala mihemko na kuwa muda ukifika kitamtangaza.
Akihutubia mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Magomeni jijini hapa, Mbowe aliwaomba wananchi kuuvumilia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwa sababu viongozi wake wanaendelea na majadiliano na watakapokubaliana watamtangaza mgombea wao.
Awali, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu alisema ilikuwa wamtangaze mgombea urais kama ilivyoripotiwa na gazeti hili, lakini wenzao wa CUF wamewaomba kuwa wanaendelea na vikao vyao vya chama.


Monday, 20 July 2015

Chadema yatangaza ratiba kura ya maoni.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetangaza ratiba ya kuanza kura ya maoni ndani ya chama hicho kuwa itaanza leo (Julai 20) na kumalizika Julai 25 mwaka huu.

Kura hiyo inakuja baada ya kukamilika kwa kazi ya uchukuaji fomu za kuomba kuwania ubunge na udiwani, ndani ya chama hicho.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano Chadema, Tumaini Makene, alisema jana kuwa katika hatua hiyo, kila uongozi wa kanda umepanga ratiba yake ya kura za maoni katika majimbo mbalimbali.

Makene alisema kupitia mchakato huo wa kura ya maoni, wana wa Chadema  watapata wagombea ubunge makini ambao watakihakikishia chama ushindi kwenye Uchaguzi Mkuu, utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Alisema ili kufanikisha mchakato huo, Waratibu wa Kanda za Chama, Makatibu wa Mikoa na Makatibu wa Majimbo watoe ushirikiano kwa vyombo vya habari ili viweze kufuatilia nchi nzima na kuuhabarisha umma wa Watanzania.

Mnyika achukua fomu ya Ubunge
Wakati huo huo, Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika (pichani), jana alichukuliwa fomu na Wazee wa chama hicho wa jimbo hilo wakimshinikiza kuwania tena nafasi hiyo.
 
 Wazee hao ambao walifika kwenye ofisi za jimbo maeneo ya Kimara Kona, majira ya mchana walimtaka kuwania nafasi hiyo kwa mara nyingine.

Akizungumza na mtandao huu, Katibu wa jimbo hilo, Justine Mollel, alisema katika kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya Ubunge kwenye jimbo hilo hadi jana aliyechukua fomu ni Mnyika pekee.

Alieleza kuwa, kwenye jimbo jipya la Kibamba jumla ya makada saba wa Chadema, walijitokeza kuchukua fomu kwa ajili ya kuwania nafasi hiyo.

“Ni kweli Mnyika leo amechukuliwa fomu na Wazee wa Chadema Jimbo la Ubungo kwa ajili ya kuwania nafasi ya Ubunge na mpaka sasa hakuna aliyechukua fomu ya kuwania nafasi hiyo na anatarajia kuirudisha leo jioni (jana),” alisema Mollel.

Saturday, 11 July 2015

Wabunge Ukawa kuchagua mgombea urais

Dar es Salaam. Hatimaye leo wabunge wote wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wanakutana na viongozi wao wa jijini hapa kumchagua mgombea urais atakayeviwakilisha vyama hivyo katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25.
Mkutano huo wa wabunge umekuja baada ya vikao kufanyika mfululizo wiki hii, huku kukiwa na mvutano kuhusu nani au chama gani kisimamishe mgombea urais.
Jana gazeti hili liliripoti kwa uhakika habari zilizotoka ndani ya vikao hivyo na kuthibitishwa na Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, Dk Emmanuel Makaidi, kuwa vyama hivyo vitaweka wazi mgombea wake wa urais leo.

“Tumeshakubaliana namna ya kugawana kata na majimbo 13 yaliyobaki na Jumamosi tutaweka wazi kwa wananchi. Pamoja na hilo pia tutamtangaza mgombea urais na chama anachotoka,” alisema Dk Makaidi.

Friday, 10 July 2015

UKAWA WASHIRIKI FUTARI YA PAMOJA

Katibu Mkuu wa CHADEMA Dkt. Willibroad Slaa akishiriki futari iliyoandaliwa na Ofisi ya Kambi ya Upinzani Bungeni wakati wa kikao cha Viongozi Wakuu wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) na wabunge wa umoja huo kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam kujadili mikakati mbalimbali ya ushindi kuelekea uchaguzi mkuu. Kushoto kwake ni Mbunge wa CUF, Ali Khamis Seif (Mkoani) na kushoto kwake ni Naibu Katibu Mkuu wa NLD Zanzibar, Ahmad Hemed.