Kuanzia tarehe 18/06/2015.
Ni tarehe za kujiandikisha kupiga kura kwa wakazi wa Manundu,
Kilole,Old Korogwe, Mtonga, Kwamsisi, Mgombezi,kwandolwa na magunga.
Napenda kuchukua fursa hii kukusihi Mwana Korogwe mwenzangu ujitokeze
kwa wingi kuandikishwa katika vituo vyitakavyokuwepo karibu na eneo
unapoishi. Nakusihi kutumia fursa hii Muhimu kwa wote wenye umri wa
kupiga kura na wale wanaotarajia kufikisha umri wa miaka 18 ifikapo
mwezi wa kumi mwaka Huu. Kumbuka Kuwa Mwaka Huu ni mwaka wa mabadiliko
tukatae. Rushwa ya Kanga,pesa na vitenge ili utu wetu uthamaniwe.
********************************************************************************************************************
HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA WIZARA
YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI MHE. SUSAN ANSELM JEROME LYIMO (MB),
AKIWASILISHA BUNGENI MAONI YA KAMBI YA UPINZANI KUHUSU BAJETI YA WIZARA
HIYO KWA MWAKA WA FEDHA 2015/2016
Inatolewa chini ya Kanuni ya
99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Aprili, 2013
_______________________
1. UTANGULIZI
Mheshimiwa spika,
napenda kuchukua fursa hii adhimu kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema
kwa kunijalia afya njema na kuweza nkusimama hapa kusoma hotuba hii. Kipekee namshukuru sana Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Mhe. Freeman Mbowe kwa kuendelea
kuniamini katika kusimamia Wizara hii nyeti kwa maendeleo ya Taifa. Aidha, nawapongeza
kwa dhati wenyeviti wenza wa UKAWA; Mhe. Dkt. Emanuel Makaidi wa NLD, Mhe. Prof.
Ibrahim Lipumba wa CUF na Mhe. James Mbatia wa NCCR Mageuzi kwa kazi kubwa sana
na nzuri wanayofanya ya kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa
kujiunga na UKAWA kwa kuwa ndio tumaini pekee
lilobaki la kuwakomboa na ndio njia pekee ya kuiondoa serikali ya CCM madarakani ifikapo 25/10/2015. Hivyo
naomba wananchi wote wanaokerwa na kuporomoka kwa shilingi yetu, ufisadi,
rushwa na hali mbaya ya maisha watumie fursa hii ya maboresho ya Daftari la
Kudumu la Wapiga Kura, kujitokeza kwa wingi na kuwahi kujiandikisha mapema
daftari litakapopita katika maeneo yao
kwani ndio njia pekee ya kuiondoa CCM madarakani kidemokrasia.
Inaendelea.......
Mheshimiwa Spika, napenda pia kutoa shukrani zangu za dhati kwa
wanawake wa Mkoa wa Kinondoni kichama kwa ushirikiano wao, kipekee nawashukuru
viongozi wa CHADEMA na wanachama wa Jimbo hilo kwa ushirikiano mnaonipatia katika
kutimiza nia na ndoto zangu. Mungu awabariki sana.
Mheshimiwa Spika, kwa
kuwa maisha ya Bunge hili la kumi yatafikia ukomo wake hivi karibuni, hii
itakuwa ni hotuba yangu ya mwisho kama Msemaji
Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi. Hata hivyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni itakumbukwa kwa kwa jitihada zake za kuikosoa
na kuishauri Serikali juu utekelezaji wa majukumu ya Wizara hii kwa lengo na
nia nzuri ya kuboresha elimu hapa nchini. Ni imani yangu kwamba niliitumikimia
nafasi hii ya Waziri Kivuli wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa uaminifu na weledi
mkubwa. Na ni furaha yangu vilevile kwamba wananchi na wadau wote wa elimu
waliridhika na mchango wa kazi za
upinzani katika wizara hii.
2. SERIKALI YA CCM ILIVYOSHINDWA
KUTEKELEZA ILANI YAKE KUHUSU ELIMU
Mheshimiwa Spika, Serikali hii ya awamu ya nne ya CCM imeshindwa kutekeleza Ilani yake ya
Uchaguzi kuhusu Elimu kwa mihula yote miwili ya utawala wake. Ibara ya 85 ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya
mwaka 2010 inasema kwamba: “Serikali
itachukua hatua za kuboresha, kuimarisha
elimu ya awali hadi ya Chuo Kikuu na kuhakikisha kwamba elimu ya ngazi zote
itakayotolewa nchini tangu sasa iwe na ubora
utakaowawezesha vijana wetu kuchukua nafasi zao stahiki katika Jumuiya ya Afrika
Mashariki na dunia kwa ujumla”.
(a)
Elimu ya Awali
Mheshimiwa Spika, Chama
cha Mapinduzi (CCM) kiliwaahidi watanzania kupitia Ilani yake ya uchaguzi kufanya
yafuatayo katika Elimu ya Awali endapo kitapewa ridhaa ya kuongoza Serikali.
i.
Kuhakikisha
kwamba kila shule ya msingi ina darasa la Elimu ya Awali lenye madawati yanayolingana na hali ya
watoto wa elimu hiyo.
ii.
Kujenga
vyoo kwa ajili ya watoto wa Elimu ya Awali ili wasiingiliane na wale wa shule
ya msingi.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya
Upinzani inapenda kuwaambia wananchi wote kwamba walitapeliwa na CCM kwani Serikali ya CCM haikutekeleza ahadi
hiyo hata japo kwa asilimia 50. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka
Serikali kulieleza Bunge wananchi kama imetekeleza ujenzi wa madarasa ya elimu
ya awali katika kila shule ya msingi nchini
na kuweka madawati yanayolingana na watoto hao, sambamba na ujenzi wa
vyoo vya watoto wa elimu ya awali katika kila shule ya msingi ili wasiingiliane
na wale wa shule ya msingi kama ilivyoahidi.
Mheshimiwa
Spika, mazingira ya elimu ya awali bado yako duni sana ambapo asilimia
kubwa ya watoto bado wanakaa chini. Aidha kumekuwa na ongezeko la matatizo ya
kukosa matundu ya vyoo, kukosa chakula jambo linalowafanya watoto kukosa hamasa
ya kujifunza kutokana na njaa, na vifaa duni vya kufundishia na kujifunzia.
Mheshimiwa Spika, Uwiano
wa mwalimu kwa wanafunzi kwa elimu ya awali nao umekuwa ni tatizo. Japo lengo
la kitaifa ni mwalimu 1 afundishe wanafunzi 25, hali ya uwiano wa kitaifa ni
mbaya sana ambapo takwimu za BEST za mwaka
2013 zinaonesha uwiano hivi sasa ni mwalimu 1 anafundisha wanafunzi 199 na kila
mwaka unaongezeka ambapo mwaka 2010 ulikuwa 1:73 ukaendelea kukua na kufikia
1:124 mwaka 2012, na sasa umefika 1:199
(b) Elimu ya Msingi
Mheshimiwa Spika, katika kuboresha elimu ya msingi, Chama cha
Mapinduzi pia kiliwaahidi wananchi kufanya yafuatayo endapo kingepewa ridhaa na
wananchi kuongoza Serikali:
i.
Kuendelea
kuyaboresha maslahi ya walimu ili kuhakikisha mishahara itolewayo inazingatia
hali halisi ya maisha na soko.
ii.
Kuendelea
kuimarisha ukaguzi wa shule na kuhakikisha kila shule inakaguliwa angalau mara
moja kwa mwaka na taarifa ya ukaguzi kufanyiwa kazi.
Mheshimiwa Spika, wananchi waliamini, wakaichagua CCM kuongoza dola.
Lakini baada ya kushika dola wamesahau kabisa yote waliyoahidi. Wote tunajua madhila yanayowapata
walimu wetu. Kilio chao cha malimbikizo
ya mishahara na stahili zao nyingine ni
cha muda mrefu sana.
Jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba hata mishahara ya walimu imekuwa haifiki kwa wakati. Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni imebaini kwamba baadhi ya walimu walioajiriwa tarehe 1 Mei, 2015
hawajalipwa fedha yao
ya kujikimu (settling in allowance) hadi leo.
Mheshimiwa Spika, kama tulivyosema walimu ndio nyenzo kuu katika
elimu lakini cha ajabu walimu wa Tanzania
wamekuwa wakionewa na kudhalilishwa kila leo. Mfano Serikali imetoa
muundo mpya wa mishahara ya walimu Julai, 2014 unaojulikana kama
TGTS ambapo zaidi ya walimu laki moja (100,000) walipaswa kutoka E kwenda F. Walimu hawa kwa makisio ya chini wanahitaji
zaidi ya bilioni mia moja (100,000,000,000/=) kwa wastani wa nyongeza ya
shilingi 100,000/= kwa mwezi. Kwa
mahesabu rahisi kama ni walimu 100,000 x
100,000/= kwa miezi 12 kwani muundo huu umeanza toka Julai, 2014.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali
kuonyesha fedha zilizotengwa kwa ajili ya nyongeza ya mishahara ya walimu
katika bajeti hii. Msingi wa hoja hii ni kuepuka mwendelezo wa malimbikizo ya
madeni ya walimu ambayo licha ya kuwa kero kwa walimu sasa pia yameanza
kutumiwa kama kete ya kisiasa nyakati za
chaguzi. Nathubutu kusema hivyo kwa
sababu Rais Kikwete akizungumza na chama cha walimu hivi karibuni alisema kabla
hajaondoka madarakani atahakikisha walimu wamelipwa madeni yao kana kwamba hakuyaona madeni hayo tangu
2005 alipoingia madarakani. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali pia
kulieleza Bunge hili kama lile deni ambalo Serikali ilisema inalihakiki na kwamba
sasa ni bilioni 10 lipwa lini na tengeo lake katika
bajeti hii liko wapi? Aidha Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua wale
walimu zaidi ya 37,000/= waliopandishwa madaraja lakini hawajarekebishiwa
mishahara yao
watalipwa lini?
Mheshimiwa Spika, kuhusu ukaguzi; ni wazi kuwa bila ukaguzi ubora
wa elimu hauwezi kupatikana. Licha ya majigambo na ahadi hewa ya Serikali hii
kupitia Ilani ya CCM; kwamba kila shule itakuwa inakaguliwa mara moja kwa
mwaka, takwimu za wizara zinaonesha kwamba, ukaguzi wa shule umefikia asilimia
37 tu. Hii ina maana kwamba zaidi ya asilimia
63 ya shule za Msingi na sekondari hazikukaguliwa.
Mheshimiwa Spika, Serikali hii ya CCM ni ya ajabu sana kwa kuwa imechoka, inajichanganya na imefikia
hatua ambayo hata haina kumbukumbu ya mambo iliyowahi kuahidi. Nasema hivi kwa
sababu tarehe 29 Aprili, 2013, Rais Jakaya Kikwete aliwaahidi wananchi
kupitia mazungumzo yake na Wakuu na Wamiliki wa Shule za Sekondari binafsi huko
Mbeya kwamba “Serikali ingeanzisha Wakala wa Ukaguzi anayejitegemea na kwamba
Serikali ingemwezesha Wakala huyo kwa rasilimali fedha /watu na vitendea kazi
ili kimarisha utendaji kazi ya ukaguzi na matokeo yake yataonekana kwa muda
mfupi”,
Mheshimiwa Spika, jambo hilo
halijafanyika, lakini mbaya zaidi ni kwamba Kambi Rasmi ya Upinzani
imesikitishwa sana
na utendaji wa serikali hii baada ya ofisi ya Waziri Mkuu kuandika barua ya kumbukumbu No: CBC/10/348/05/10 ya tarehe
13 Oktoba, 2014 inayositisha agizo la Rais la kuanzisha wakala wa ukaguzi wa
shule. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka Serikali kutoa maelezo juu ya
mkanganyiko (confusion) huu ndani ya Serikali kuhusu uanzishwaji wa wakala wa
ukaguzi wa shule. Swali la kujiuliza tuna serikali ngapi??
Mheshimiwa Spika, napenda kumalizia sehemu hii kwa kuwaambia
wananchi kwamba, Elimu haijawahi kuwa kipaumbele katika sera za CCM kwa awamu
zote nne za utawala wake ndio maana haitekezi hata ilani yake yenyewe . Sera ambayo CCM imepigia upatu kwa miaka yote
53 ya uhuru na ambayo pia imeshindwa kutekeleza ni Kilimo. Ndio maana tangu
enzi za uongozi wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere sera zilizosikika ni Siasa
ni Kilimo, Kilimo cha Kufa na Kupona , Kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa, na
sasa Kilimo Kwanza. Hatujawahi
kusikia Elimu Kwanza kwa utawala wa
CCM kwa miaka yote 53 ya uhuru.
Mheshimiwa Spika, Sera ya Elimu Kwanza ni Sera ya Upinani. Ipo katika Ilani ya Uchaguzi
ya CHADEMA ya 2005, na 2010 na imepewa kipaumbele cha kwanza, cha pili na cha
tatu. Na kwa kuwa sasa hivi tupo katika ushirikiano
wa UKAWA, sera hii imekuwa ni Sera ya UKAWA. Hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inawaonya wanaotangaza nia ya kugombea Urais wa Tanzania
kupitia CCM kuacha kuwawadanganya wananchi kwamba Elimu itakuwa kipaumbele
namba moja ikiwa watachaguliwa, kwa kuwa walikuwa Serikalini kwa miaka yote
tangu uhuru na wakashindwa kufanya hivyo.
Mheshimiwa Spika, Itakumbukwa kwamba CHADEMA iliposema elimu
itakuwa bure kama ingechaguliwa kuunda
Serikali mwaka 2005 na 2010, CCM iliendesha propaganda chafu na kuwapotosha
wananchi kwamba haiwezekani kutoa elimu bure. Lakini ili kuthibitisha ile
methali isemayo kwamba njia ya mwongo ni
fupi, CCM sasa hivi imekubali kula matapishi yake na kusema katika
kipengele cha 3.1.5 cha Sera Mpya ya elimu ya mwaka 2014 kwamba Elimu ya Msingi
itakuwa bure. Huu ni uthibitisho kwamba
CCM imebobea katika wizi hadi kufikia hatua ya kuiba sera za upinzani waziwazi
bila aibu!!! Lakini inathibitisha kwamba Sera za Upinzani zinatekelezeka, na
kwa maana hiyo, UKAWA ukitwaa madaraka ya dola katika uchaguzi wa Oktoba, 2015
Elimu ya Msingi mpaka Chuo Kikuu itakuwa BURE KWELI KWELI.
2. SERA
MPYA YA ELIMU 2014
Mheshimiwa Spika, Sera ya Elimu ilizinduliwa kwa mbwembwe nyingi
lakini ukiisoma vizuri sera ile ni vituko vitupu. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilidhani
kwamba, baada ya Sera ya Elimu ya 1995 kuwa na mapungufu mengi yaliyopelekea
mambo mengi kuharibika basi ingekuwa somo tosha kwa maboresho ya sera hii, lakini
kwa masikitiko makubwa sera hii imekuwa
ni ya matamko tu.
Mheshimiwa Spika,
tumekuwa tunashindwa kutekeleza sera zetu kwa
kuwa zimekuwa ni sera bainishi (substantive policies) na hivyo
kubainisha mapungufu
tu na kuacha sehemu ya pili ya utekelezaji.
Hivyo kilichobainishwa kinashindikana kutekelza kwa kuwa nyenzo za
utekelezaji haziwekewi
mkazo. Kimsingi, ili sera hii
itekelezeke ni lazima iwe na ngazi hizi
mbili yaani sera bainishi na sera namna. Sera nyingi hapa nchini
zimekuwa dhaifu na kutokutekelezwa kwa kukosa ngazi ya pili yaani sera
namna.
Mheshimiwa
Spika, Ili sera hii ya elimu iweze kutekelezeka inahitaji
kutafutiwa ufumbuzi wa mambo matatu la sivyo hakutakuwa na jipya. Mambo hayo ni
pamoja na walimu bora, zana
bora za kufundishia, na walimu wenye motisha. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka
Serikali kulieleza Bunge hili imetenga fedha kiasi gani katika bajeti hii kwa
ajili ya zana bora za kufundishia na motisha kwa walimu ili kurahisisha
utekelezaji wa Sera Mpya ya Elimu?
Mheshimiwa Spika, Tanzania imekuwa inasifika sana kwa kuandika vizuri sera zake lakini
utekelezaji wake ni Shiidaa!!! Mfano sera
hii haielezi ni kwa kiasi gani itaondoa ubaguzi au matabaka ya elimu hasa
viwango vya elimu. Aidha, haielezi nini
maana ya kufuta ada ikiwa kuna michango ni mingi kuliko ada yenyewe.
Mheshimiwa Spika,
Sera ya Elimu inasema serikali itahakikisha kuwa elimu ya msingi katika mfumo wa umma inatolewa bila ada.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulithibitisha Bunge hili kama elimu bila ada itaanza kutolewa kwa mwaka wa fedha
2015/16, au tamko hili la sera lilikuwa ni la kisiasa kwa ajili ya kuendelea
kuwahadaa watanzania?
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inatiaka Serikali kutoa majibu kwa swali hili kwa sababu asa hivi wazazi wengi
wana mkanganyiko wa suala hili kwa kuwa
wanafahamu kuwa kwa kuwa sera hii imezinduliwa mwezi Februari 2015 na matarajio
yao ni kwamba utekelezaji wa elimu bure utaanza mwaka wa fedha 2015/2016.
Mheshimiwa
Spika, Katika kujibu hoja hii, Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inaitaka serikali ikumbuke kuwa
changamoto kubwa za mazingira ya kufundishia na kujifunzia zinatokana na ufinyu
wa bajeti na pia serikali kutotoa fedha za kutosha shuleni. Mathalani katika utekelezaji wa MMEM I na MMEM II ni
wastani wa shilingi 5,000 hadi shilingi 6,000 kati ya shilingi 10,000 kwa kila mwanafunzi
ndio zilitolewa na serikali na hata katika MMEM III bado serikali imeshindwa
kutoa fedha hizi. Aidha, katika mwaka wa fedha 2014/2015 serikali imetoa
wastani Shilingi 860 tu, kwa kila
mwanafunzi badala ya shilingi 10,000. Kambi Raasmi ya Upinzani inaitaka Serikali
kueleza ni kwa kiwango gani changamoto hizi zinapatiwa ufumbuzi katika bajeti
ya 2015/2016 au ndio kusema Bussiness as Ussual.
3. SHULE
BINAFSI
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na malalamiko mengi sana kuhusu gharama za shule za binafsi kuwa
kubwa mno kiasi kwamba ni wananchi wachache wanaweza kuwalipia watoto wao ada
na gharama nyingine katika shule hizo.
Na kwa kuwa shule hizo zinatoza ada kubwa zinakuwa na uwezo wa kuwapa
motisha walimu na kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunza hivyo
kuonekana kwamba zinatoa elimu bora kuliko zile za Serikali.
Mheshimiwa Spika, jambo hili limeleta matabaka katika utoaji wa
elimu kwani sasa inaonekana kwamba shule za Serikali ni kwa ajili ya watu
masikini na shule binafsi ni kwa ajili ya watoto wa matajiri. Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili imefanya jitihada gani
katika kuwianisha gharama za elimu kati ya shule binafsi na shule za Serikali
ili kuondoa matabaka katika utoaji wa elimu? Kwa kuwa wenye shule binafsi
wanadai gharama zao ziko chini kama
tutaangalia Student’s Unit Costs. Je pamoja na malalamiko hayo ni kwa nini
serikali haijafanya utafiti kujua kama hili ni kweli Ili
wananchi wajue gharama halisi za elimu? .
4. SERIKALI
YA CCM ILIVYOSHINDWA KUWAPATIA WANAFUNZI MADAWATI MASHULENI TANGU UHURU
Mheshimiwa Spika, ni jambo la kusikitisha na ni aibu kwa Serikali
hii ya CCM inayojigamba kuwa imeleta maendeleo kushindwa kuwapatia wanafunzi
madawati licha ya utajiri wa rasilimali za misitu tulizo nazo, na licha ya
ujuzi na nguvu kazi iliyopo katika magereza yetu ambapo wafungwa na mahabusi wangeweza
kutumika kutengeneza madawati hayo.
Mheshimiwa
Spika, ni aibu kubwa kwa
Serikali hii ya CCM kujigamba katika Sera Mpya ya Elimu na Waziri Mkuu kujibu swali hapa Bungeni na
kukazia kwamba wanafunzi wa shule za msingi watapatiwa Kompyuta Mpakato
(Laptops) ilhali sehemu kubwa ya watoto wetu bado wanakaa chini na wengine wanakalia mawe kama
nyani kwa miaka 54 sasa ya uhuru. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapata tabu
kuelewa kama Serikali hii imechanganyikiwa au
iko serious kwamba itawapa kompyuta
wanafunzi wambao hawana pa kukaa shuleni na shule hizo hazina umeme.
Mheshimiwa Spika, wenzetu wa
Kenya na Rwanda wameweza
kuwapa watoto wao kompyuta mpakato (Laptops). Katika bajeti ya elimu - Kenya toka 2013
walitoa laptops kwa wanafunzi wote wa shule za msingi lakini hapa kwetu ni porojo tu. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inaitaka Serikali kuonesha bajeti ya kununua laptops kwa wanafunzi ikiwa ni
sehemu ya utekelezaji wa Sera Mpya ya Elimu na ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya
Waziri Mkuu akijibu swali hapa Bungeni kwamba wanafunzi wote wa shule za Msingi
watapatiwa kompyuta mpakato.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inahoji, hivi
Kamati Kuu ya CCM iliyokaa zaidi ya mara 212 (x4 kila mwaka) ukiacha vile vikao
vya dharura kwa miaka yote 53 na nusu ya uhuru huwa inajadili nini ikiwa hali
ya upatikanaji wa madawati ni tete kiasi hiki huku magogo yetu yakiuzwa China na
kwingineko? Kambi Rasmi ya Upinzani imeshawishika kuamini kwamba Serikali hii
ya CCM si kwamba imechoka tu bali pia imefikia ukomo wa kufikiri na kwa maana
hiyo kuiruhusu kuendelea kutawala ni kuruhusu anguko kuu la nchi au waswahili
wanasema ni janga la Taifa na ni shiiida.
5. ELIMU
YA UALIMU
Mheshimiwa Spika, Elimu ni mwalimu, kwani unaweza kuwa na madarasa
mazuri sana,
maabara ya viwango vya juu lakini bila mwalimu mwenye motisha na aliyepewa
mafunzo vizuri hakuna chochote tutakachofanikiwa. Elimu ni sawa na kiwanda
ambapo mwanafunzi ni malighafi, walimu na vitabu ndio mashine za uchakataji na
usindikaji. Hivyo kama ilivyo kwa
malighafi inapopita kwenye mashine tunachopata ni kitu kipya kama
pamba kuwa nguo. n.k. Hivyo mtoto
anaingia hajui chochote lakini anategemewa atoke amebadilika kwa kujua kusoma,
kuandika na kubwa zaidi kujitambua na kujua kuchambua mambo. Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili kama
Elimu ya Ualimu inayotolewa ina ubora wa kutosha kwa kuwa mwalimu bora ndiye anayegemewa
katika kuwafundisha watoto wetu
Mheshimiwa spika. Kulingana na mtaala wa mafunzo ya ualimu, mafunzo kwa vitendo kwa
walimu (Block Teaching Practice) yanapaswa kutolewa kwa wiki 8 kila mwaka wa
masomo. Kwa miaka miwili 2013/14 na
2014/15 mafunzo yametolewa kwa wiki 2 tu yaani wiki 4 badala ya wiki 16.
Kupunguza muda wa mafunzo kwa vitendo kunapunguza pia weledi na uwezo wa
mwalimu husika. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza Bunge
hili sababu za kupunguza muda wa mafunzo kwa vitendo na athari zitakazotokana
na muda huo kupunguzwa. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni pia inahoji, Serikali
inategemea kuwapata walimu wa kiwango gani cha weledi ikiwa inapunguza muda wao
wa mafunzo?
Mheshimiwa Spika, Bunge lako Tukufu kwa kutambua umuhimu na ubora wa waalimu lilipitisha
bajeti ya shilingi 7,210,370,000/=
(2014/2015). Serikali kwa kutothamini fani hii ilipunguza kiasi hicho kwa
shilingi 5,165 006, 020, sawa na 72%,
hii ina maana kwamba fani ya Elimu ya Ualimu wamepata shilingi bilioni 2 tu sawa na asilimia 28% ya
fedha zilizoidhinishwa na Bunge kwa mwaka huo hadi April 2015.
Mheshimiwa Spika, inasikitisha na inatia hasira kusikia kwamba
Serikali inasema mkakati Iliyo nao ili kuhakikisha walimu hawa waliokosa
mafunzo kwa vitendo, “watakuwa chini ya uangalizi wa wakaguzi wa shule kwa
kipindi cha mwaka mmoja pindi
watakapoajiriwa ili kupata muda wa kutosha wa mazoezi ya ufundishaji” Kambi
Rasmi ya Upinzani inaihoji Serikali itatekeleza vipi mpango huo wa ukaguzi na
kwa bajeti ipi ikiwa ukaguzi uliofanyika ni asilimia 30 tu?
6. ELIMU
YA JUU
Mheshimiwa Spika, elimu ya juu ndio inayomfunza kijana jinsi ya
kuchambua mambo na kujenga weledi katika fani mbalimbali. Mwl. Nyerere, katika kitabu chake cha Uhuru na
Maendeleo, alisema: “Intellectuals have a special contribution
to make to the development of our nation, and their knowledge and greater understanding
that they should posess, should be used
for the benefit of the society of which we are all members”
Mheshimiwa Spika, Kinyume na maneno ya Hayati Baba wa Taifa, mchango
wa wasomi wetu katika maendeleo ya jamii na taifa kwa jumla umewekewa vikwazo
na mfumo wa utawala wa Serikali hii ya CCM. Wasomi wenye elimu ya juu kokosa
ajira limekuwa ni jambo la kawaida, na wasomi pia kukosa fursa na mazingira bora ya kujiajiri
nayo ni changamoto kubwa.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali
hii ya CCM kueleza imewasaidiaje wahitimu wa elimu ya juu kama
vile wahandisi, kilimo, wanasheria, katika kuanzisha Kampuni zao za uhandisi,
Kampuni za huduma za kisheria (Law firms), Kampuni za ushauri nasaha kwa
waliohitimu fani za Saikolojia nk. Nauliza hivi kwa sababu kodi za wananchi
zimetumika kuwasomesha wahitimu hao lakini mwisho wa siku wanabaki mitaani bila
tija yoyote. Hii inamaana kwamba Taifa limeingia hasara kuwasomesha watu ambao
hatimaye hawana mchango wowote katika uchumi wa nchi na badala yake wanakuwa
tegemezi na kuongeza kiwango cha umasikini nchini. Na haya yote yamesababishwa
na mitaala mibovu ya elimu ambayo imeshindwa kuwajengea uwezo wa kujiajiri pale
wanapokosa ajira za moja kwa moja.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali
kulieleza Bunge hili, nchi hii inafuata falsafa gani ya elimu kwa sasa? What is our current education philosophy? Nauliza
hivi, Mhe. Spika, kwa sababu wakati wa utawala wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere, nchi hii ilikuwa ikifuata falsafa ya “Elimu ya
Kujitegemea” yani Education for Self Reliance,
ambapo msingi wa elimu ulikuwa ni kumwezesha aliyenufaika na elimu
kujiajiri katika sekta mbalimbali za uzalishaji mali. Lakini kwa hali ilivyo sasa,
elimu yetu haionekani kuwa na msingi wa kumsaidia mhitimu kujiajiri. Kambi
Rasmi ya Upinzani inataka kujua kama ile falsafa ya elimu ya kujitemea
imefutwa, na kama imefutwa sasa hivi taifa
lina falsafa gani ya elimu au tupo tupo tu?.
7. MATATIZO
YA ELIMU YA JUU
Mheshimiwa Spika, elimu katika ngazi zote nchini imepanuka kwa kasi isiyozingatia ubora.
Hii inadhihirishwa na utafiti uliofanywa na The Global competitiveness Index
(GCI) mwaka 2013/14 kuangalia ubora wa vyuo vikuu kwa nchi 148
duniani. Matokeo yanaonesha Kenya
ikishika nafasi ya 44, Uganda
ya 82, huku Tanzania ikishika nafasi ya 100.
Mheshimiwa Spika, pamoja na tafiti kuonyesha Tanzania
tulivyo nyuma katika ubora wa elimu ya Juu, sasa hivi kumezuka tatizo kubwa la
utofauti wa mitaala ya Vyuo Vikuu hususan vile vya binafsi hali inayopelekea
migomo na sintofahamu miongoni mwa wanafunzi. Mfano mzuri ni vyuo vya St. Joseph na Kampala
International University (KIU). Kwa muda mrefu tatizo hili limefikishwa kwa
wahusika na bado ufumbuzi wa kina haujajulikana. Tunaitaka serikali itueleze uswahiba uliopo
kati yake na Vyuo hivi. Na ni kwa nini
wanafunzi wakitanzania wateseke kwa manufaa ya wamiliki?
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema
hapo awali, kumekuwa na tofauti kubwa ya mitaala ya Elimu ya juu kati ya vyuo
vya elimu ya juu vya Serikali na vyuo binafsi. Tofauti hii kubwa kwa upande
mmoja imesababishwa na kuongezeka kwa kasi kwa vyuo vya Elimu ya juu nchini
kutokana na ongezeko la watu wanaohitaji elimu lakini kwa upande mwingine
tofauti hii imesababishwa na ukweli kwamba elimu hasa kwa vyuo binafsi inatolewa
kibiashara zaidi kuliko huduma. Kutokana na hali hii ya vyuo vya elimu ya juu
(hasa vya binafsi) kuwa katika mkakati wa kufanya biashara zaidi kuliko kutoa
huduma ya elimu, imesababisha baadhi ya vyuo kuongeza muda wa programu zake
kutoka miaka minne hadi minne na miezi sita, na miaka hadi mitano na miezi sita bila kuzingatia utaratibu
wa bodi ya mikopo. Tunataka serikali itueleze hili ongezeko la miezi sita
litagharamiwa na nani huku wataalamu wa
bodi wakidai kutotambua muda huo wa nyongeza?.
Mheshimiwa
Spika, hali hii
imesababisha pia baadhi ya vyuo kujitengenezea mitaala yake kwa lengo la
kuwavutia wanafunzi kwa kile kinachoitwa “bridging courses”na hivyo kutanua
wigo wa kujipatia faida zaidi bila
kuzingatia ubora wa elimu inayotolewa na bila kujali namna elimu iliyotolewa
inavyoendana na mazingira ya nchi yetu. Kutokana na hali hii, vijana wengi
wanaohitimu ngazi mbalimbali katika elimu ya juu wamekuwa wakishindwa kuingia
katika soko la ajira kwa kuwa masomo waliyofundishwa hayaendani na mahitaji
halisi ya soko la ajira; Mfano ni wahitimu wa Astashahada ya famasi ya Kampala International University.
Mheshimiwa
Spika, kwa kuwa kumekuwa na utofauti mkubwa wa mitaala katika
vyuo vya elimu ya juu jambo linalosababisha
kukosekana kwa ubora linganifu wa elimu ya juu katika ngazi mbalimbali; na
kwa kuwa kukosekana kwa ubora linganifu
wa elimu ya juu unaozingatia mazingira ya nchi yetu kumesababisha vijana wengi
wanaohitimu elimu ya juu katika ngazi mbalimbali kukosa sifa za ushindani
katika katika soko la ajira na hivyo kukosa fursa mbalimbali za ajira; na kwa kuwa udhaifu wa mitaala katika elimu ya juu umesababisha mara kadhaa
migogoro kati ya wanafunzi na watawala wa vyuo husika na hivyo kusababisha
baadhi ya wanafunzi kusimamishwa masomo na kufukuzwa kabisa; na kwa kuwa Tume
mbalimbali zilizoundwa kuchunguza ubora wa elimu hapa nchini zilibaini kuwa
elimu ya Tanzania imekuwa ikiporomoka mwaka hadi mwaka; na kwa kuwa kati ya sababu zilizotajwa za kuporomoka kwa
elimu ni kukosekana kwa mitaala thabiti inayoeleweka na inayozingatia ubora wa
elimu katika mazingira mahalia; na kwa kuwa Tume ya Elimu ya Juu (TCU) ina
mamlaka ya kuratibu na kusimamia mitaala
ya vyuo vya Elimu ya Juu;
HIVY0
BASI, Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kufanya yafuatayo:
i.
Kuiagiza Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) kutoa ndani
ya kipindi cha siku sitini, mwongozo mpya kwa vyuo vya elimu juu nchini kuhusu
ya vigezo vya kuzingatia wakati wa kuandaa mitaala ya elimu ya juu.
ii.
Kuvifungia
mara moja vyuo vyote vya Elimu ya Juu
vinavyoendeshwa kwa maslahi ya kibiashara zaidi bila kuzingatia mitaala
na ubora wa elimu mpaka hapo vitakapojirekebisha;
iii.
Kuiagiza
Tume ya Vyuo vikuu nchini (TCU) kusitisha mara moja kutoa ithibati kwa vyuo vya
Elimu ya Juu ambavyo vitakuwa havina mitaala iliyozingatia vigezo
vitakavyowekwa na Tume ya Elimu ya Juu.
iv.
Kuhakikisha
muda wa Provisional Accredation ni wa kipindi cha mwaka mmoja tu ili kuondoa
athari kwa wanafunzi wetu.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuleza ni kwa nini
Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU) ilitoa ithibati kwa Chuo Kikuu cha Kampala International
University huku wakijua baadhi ya
program hazijasajiliwa na Board mbalimbali kama
ile ya Pharmacy hivyo kusababisha hasara kwa Chuo na wanafunzi? Aidha, Kambi
Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa majibu kwa maswali yafuatayo:
i.
Ni kwa nini baadhi ya program
zinazofanana mfano Medical Laboratory na Pharamacy kwa Chuo Kikuu cha Kampala
Internationa University (KIU) zitofautiane
kwa kiasi kikubwa hivyo na Vyuo Vikuu vingine kama
Muhimbili, KCMC nk? Mfano wakati KIU
wana kozi 14 wenzao wana 7 – 8 tu?
ii.
Ni kwanini TCU na Wizara wanapopata
taarifa za matatizo haya hawajali na kuacha jambo hilo
liote mizizi na kuleta athari kubwa kama ilivyotokea KIU, St.
Joseph na IMTU?
iii.
Ni kwa nini inapotokea tatizo na
kuonyesha wazi Serikali ndio yenye makosa wanafunzi ndio wanakuwa wahanga
badala ya Serikali kuwajibika?
8.
BODI YA MIKOPO YA ELIMU YA JUU
Mheshimiwa Spika,
tangu sheria ya Bodi ya Mikopo kuanzishwa, bado
kumekuwa na changamoto nyingi kuhusu mikopo ya elimu ya juu hadi Rais
alipoteua Tume chini ya Prof. Maboko Makenya kushughulikia matatizo ya
mikopo ya Elimu ya Juu. Kinachotushangaza ni kwamba ripoti ya Tume hiyo
haijawekwa hadharani na bado matatizo ya mikopo kwa wananafunzi wa elimu
ya juu
yako pale pale. Wanafunzi wengi hawapati fedha kwa wakati hali inayoleta
adha
kubwa kwa wanafunzi kwani wengi wao wanatoka kwenye familia duni. Kwa
mfano
wanafunzi wanaosoma kozi ya ualimu katika Chuo Kikuu cha St.
Joseph, hawajalipwa fedha zao za mkopo tangu mwezi
Machi 2015 jambo linalowafanya waishi
maisha ya dhiki na hivyo kushindwa kusoma. Kinachoshangaza ni kwamba wenzao wa
Uhandisi wamelipwa. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kueleza
ni kwa nini inatoa mikopo kwa ubaguzi? Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka
Serikali kutoa maelezo ni kwa nini Chuo cha St. Joseph kiliwafukuza wanafunzi hao waliokosa mikopo na kuvumilia
zaidi ya siku 50, na ni nini hatima ya wanafunzi hao?
Mheshimiwa Spika, kuhusu urejeshwaji wa mikopo ya elimu ya juu, imebainika
kwamba urejeshaji ni mdogo sana
kwa kuwa hakuna mfumo mzuri unaoratibu zoezi la ukopeshaji na urejeshaji wa
mikopo ya elimu ya juu. Kwa muda mrefu Kambi Rasmi ya Upinzani imekuwa
ikishauri kazi hiyo kufanywa na mabenki yetu lakini mpaka sasa ushauri huo
haujatekelezwa. Tunaitaka Serikali
kulieleza bunge hili kama Bodi ya Mikopo ina
wataalamu wa mikopo kwa ajili ya kazi hiyo. Ili
kuyapatia ufumbuzi matatizo ya mikopo ya elimu ya juu, Kambi Rasmi ya Upinzani
inaitaka vilevile Serikali kutoa ripoti ya tume ya Profesa Maboko ambayo
ilipewa jukumu la kutafuta vyanzo vya matatizo na kupendekeza namna ya
kukabiliana na matatizo ya mikopo ya elimu ya juu.
Mheshimiwa Spika,
Kwa kuwa
tumeshauri mara kadhaa kuhusu matatizo ya mfumo wa mikopo ya elimu ya Juu na
kupuuzwa. Serikali Mpya ya UKAWA italipa kipaumbele suala la mikopo ya elimu ya
juu kwa kutambua kwamba mikopo ni haki ya wanafunzi na bila mikopo hiyo
hawataweza i kusoma kwa utulivu na kuzifikia ndoto zao.
Mheshimiwa Spika, Kama Serikali
haitaki ushauri wa UKAWA basi basi walau ijifunze kutoka nchi jirani ya Rwanda inavyofanya kuhusu mikopo ya wanafunzi wa
Elimu ya juu. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kueleza
yafuatayo:
i.
Ni
kwanini haitoi fedha ya mikopo hadi wanafunzi wagome na kuandamana?
ii.
Ni wapi fedha hizo zinakwenda hasa ukizingatia
100% ni za ndani?
iii.
Ni kwa nini ndani ya masaa 12 tu ya mgomo wa UDSM
19/5/2015 fedha zikatoka? Au ni sera ya
CCM kuwajengea wanafunzi tabia ya kupata haki zao kwa migomo na baadaye kusema
ni UKAWA wanachochea migomo vyuoni?
9. UWEKEZAJI
KATIKA ELIMU NA MPANGO MATOKEO MAKUBWA
SASA (BRN).
Mheshimiwa
Spika, Takwimu mbalimbali za ripoti ya utekelezaji wa
BRN ya Presidential Delivery Bureau na Jarida la HakiElimu la hali ya
utekelezaji wa BRN zinaonesha kuwa mwaka wa kwanza wa utekelezaji wa BRN
ulikuwa na changamoto nyingi za kiutekelezaji na mambo mengi yanayohusiana na
fedha hayakutekelezwa. BRN ya Elimu ilibaninisha wazi kutoa ruzuku ya asilimia
100 yaani shilingi 10,000/= kwa kila
mwanafunzi shule za msingi na shilingi 25,000/= kwa shule za sekondari lakini utekelezaji
umekuwa kwa asilimia 42 tu kwa msingi na
asilimia 48 tu kwa sekondari.
Mheshimiwa
Spika, ujenzi wa miundombinu haukutekelezeka pia
ambapo kati ya shule 792 zilizopangwa kufanyiwa ukarabati hadi ifikapo mwezi
March 2014, ni shule 56 tu zimekarabatiwa. Lengo la utoaji mafunzo ya usimamizi
kwa walimu wakuu halikutekelezwa ipasavyo ambapo kati ya walimu 19,035
waliotarajiwa kupata mafunzo ifikapo September 2013, ni walimu 3,469 tu sawa na
asilimia 18 ndio wameshapatiwa mafunzo.
Mheshimiwa
Spika, dhamira ya BRN kutatua mgogoro wa walimu na
kufanya walimu wafundishe ipasanyo ilikuwa ni nzuri hasa kwa kutoa motisha kwa
walimu na kulipa madeni ya walimu. Wakati BRN inaanza asilimia 53 ya walimu
walikuwa hawapo darasani yaani hawafundishi. Utafiti wa Shirika la Twaweza
kwenye kijarida namba 13 cha mwaka 2014 unaonesha kuwa hivi sasa ni asilimia 34
tu ya walimu ndio wanaingia na kufundisha muda wote wa kipindi na idadi
iliyobaki ama wanaingia kwa muda mfupi tu au hawaingii kabisa. Kwa takwimu hizi
za utekelezaji, Kambi Rasmi ya Upinzani
bungeni inauliza: ni mambo gani yaliyofanya sekta ya elimu hadi
kuipatia sekta hiyo alama 81 katika utekelezaji ilihali katika malengo yote ya
BRN ya elimu hakuna hata lengo moja ambalo limetekelezwa kwa zaidi ya asilimia
20? .
Mheshimiwa Spika, ni wazi Serikali haijawekeza vya kutosha katika elimu. Hii
inadhihirishwa na bajeti zetu. Kwa mfano
mwaka 2014/15 Kenya ilitenga sh Bilioni 294.6 sawa na asilimia 27.3% ya bajeti
yake kwenye elimu huku Tanzania
ikitenga shilingi 3.46 bilioni sawa na asilimia 17 ya bajeti kuu kwenye
elimu. Lakini ieleweke hata hizo
zilizotengwa ni asilimia kidogo zilizokwenda kwa wastani wa 50 au chini hadi
Machi 2015. Lakini takwimu zinaonesha
kuwa katika nchi za Afrika Mashariki Kenya
imetumia 7.8% ya GDP katika elimu huku Tanzania ikitoa 1.49 % ya GDP, Uganda 5.8% na Rwanda 4.8%. Haiwezekani usiwekeze halafu utegemee mavuno
mazuri. Ni sawa na mimea inahitaji
kuwekwa mbolea na kupaliliwa na hata kumwagiliwa. Ni jambo linalosikitisha kuona watoto wakikaa
darasani kwa miaka saba na kutoka bila chochote. Watoto hawapati chakula shuleni jambo linalowafanya
watoroke shule Jirani zetu Kenya
toka 2013 walianza program ya kula shuleni ambayo kimsingi ni motisha hasa kwa watoto wa
familia maskini.
Mheshimiwa Spika, Jambo linalochekesha ni pale Serikali hii ya CCM inapotamba kuwa
elimu imefanikiwa kwa 81% katika mpango wa matokeo makubwa sasa. Kwa mtu yeyote mwenye akili timamu atajiuliza
ni uwekezwaji gani umefanyika hadi tukapata matokeo haya. Je walimu ambao ndio watendaji wakuu wamefanyiwa
nini? Je maslahi yao,
motisha na mazingira yao
yameboreshwa? Ni jambo la kusikitisha
kuona uwekezaji ukipungua lakini matokeo yakiwa mazuri zaidi. Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inahoji; “kuna miujiza gani kama si mbinu
chafu na za ujanja ujanja kama tuliovyosema mwaka juzi? Ukweli kilichofanyika ni kubadili alama na
madaraja jambo ambalo kimsingi ni mbinu
chafu na hauoneshi uhalisia wa uwezo wa
mtoto. Ieleweke kuwa Tanzania sio kisiwa
na kwamba ukosefu wa ajira unachangiwa na ubovu wa wahitimu wetu kutokana na
mfumo wetu wa elimu na hasa mfumo mpya wa madaraja na alama.
Mheshimiwa
Spika Ni lazima tuelewe
kila mtoto wa kitanzania anahitaji elimu bora kwani elimu ni kwa ajili ya
kujikomboa na kujibadili (liberation and transformation). Ni vibaya sana kuwajaza watoto wa
maskini kwenye shule za viwango vya chini.
Kama Mwalimu Nyerere alivyosema mwaka mmoja kabla ya kifo chake (5/3 1998) akiwa Open University “Not all of us will have the same concept of community, but all of us
have a need to belong ….. nobody is asking us to love others more than we love
ourselves but those of us who have been lucky enough to receive a good
education have a duty also to help to improve the well being of the community
to which we belong, is part of loving ourselves”
Mheshimiwa
Spika, ni kwa kiasi gani
wasomi wa nchi hii na wenye madaraka
mnapenda watoto wa watanzania kupata elimu bora? Au sisi wenyewe watoto wetu
wako nje ya nchi? Je tunaboreshaje
jamii/elimu yetu kwa kuwa kufanya
hivyo ni sehemu ya kupendana? Tumeshindwa kwa kuwa tunashuhudia wasomi wetu
waliopata elimu bora wamekuwa chanzo cha kuharibu elimu yetu kwa kuruhusu akili
ndogo kutawala akili kubwa. Haiwezekani Profesa aliyepewa kuongoza sekta ya
elimu ashindwe kutoa ushauri kuhusu uboreshwaji wa elimu. Inawezekanaje
maprofesa wasajili/ watoe ithibati kwa vyuo vikuu vyenye maabara yenye kiwango
cha shule za kata? Mnategemea wahitimu wa vyuo hivi waajiriwe wapi?
10.
UCHAMBUZI WA BAJETI
Mheshimiwa Spika, pamoja na bajeti ya sekta nzima kuendelea kuongezeka kutoka Trilioni
3.46 mwaka 2014/15 hadi trilioni 3.88,
sawa na takribani asilimia 10 tu ya fedha iliyopangwa mwaka jana, si ongezeko
linaloweza kuleta mabadiliko yanayoonekana katika sekta ya elimu. Tunasema hivi
kwa kuzingatia kuwa thamani ya shilingi imeshuka na mfumuko wa bei umeongezeka.
Inawezekana ongezeko hili ni matokeo ya urekebishaji mfumuko wa bei badala ya
ongezeko halisi katika matumizi.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo uchambuzi unaonesha kuwa bado kiwango cha fedha za bajeti ya
sekta kinachopangwa ni asilimia kati ya 15 – 17 cha bajeti nzima ya serikali. Tanzania hatujaweza hata kufikia kiwango kilichokubaliwa cha
azimio la Darkar Senegal
chini ya EFA, cha kuwekeza hadi walau aslimia 20 ya bajeti ya taifa katika
elimu. Wakati tunaamini kuwa kiwango cha asilimia 17 si kibaya, lakini ni
muhimu kujua kuwa bado Tanzania
inawekeza asilimia kati ya 10-11 tu ya bajeti ya sekta ya elimu kwenye miradi
ya maendeleo ukilinganisha na majirani zetu Kenya,
Rwanda, na Uganda ambao
wamefikia walau asilimia 20 -25.
Mheshimiwa Spika, ni wazi sekta ya elimu imeendelea kupewa kipaumbele
kwa maana ya kuwa sekta inayopokea fungu kubwa zaidi la bajeti ya serikali.
Wakati ikipangiwa trilioni 3.46 mwaka jana sekta ya miundombinu ambayo
ilifuatia ilipokea takribani trilioni 2.3 wakati mwaka huu sekta ya elimu
imepangiwa trillion 3.88 wizara inayofuatia ambayo ni miundombinu imeshuka
zaidi hadi takribani Trilion 1.9.
Hatahivyo
bado kuna mapungufu makubwa ambayo inabidi yafanyiwe kazi;
Ø Kiwango cha fedha zinazokwenda kwenye matumizi ya
kawaida bado ni kubwa sana
kuliko kinachokwenda kwenye matumizi ya maendeleo ambayo ni muhimu zaidi.
Mathalani katika makadirio ya Trilioni 3.88 yanayopendekezwa mwaka huu wa fedha
kwenye sekta ya elimu, 84% zimeelekezwa katika matumizi ya kawaida huku
asilimia 16 pekee (bilioni 604) ndizo zinaombwa kwaajili ya maendeleo. Pia kati
ya Tsh bil 604 zilizopangwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo asilimia 50 ya
fedha hizi zimepangwa kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu na hivyo fedha
zinazobaki kwa ajili ya miradi halisi ya maendeleo ni ndogo sana kulingana na
changamoto zinazokabili sekta ya elimu hasa elimu ya msingi na sekondari.
Tunatoa rai kwa Wizara kuongeza fedha zaidi kwa miradi ya maendeleo
inayotekelezwa na serikali za mitaa.
Ø Tunatambua, Wizara ya Elimu imegatua madaraka na
sasa hivi shughuli nyingi za elimu ya msingi na sekondari zinatekelezwa na
serikali za mitaa na Wizara ya Elimu imebaki na jukumu la ushauri, utengenezaji
wa sera na ufuatiliaji wa utekelezaji wa sera. Cha kushangaza katika makadirio
ya bajeti ya maendeleo ya sekta ya Elimu, kati ya Sh billion 604 zilizopangwa,
sh bilioni 478.7(asilimia 79) zimepangwa wizara ya ya Elimu na Tsh bilioni 126
tu ndio zimepangwa serikali za mitaa. Swali la kuuliza inakuwaje tunapanga
fedha nyingi kwenye kazi za ushauri,utungaji wa sera na ufuatiliaji na kupanga
fedha kiasi kidogo kwenye serikali za mitaa ambazo ndio zinatekeleza shughuli
nyingi za maendeleo? Unawezaje kutatua changamoto za miundombinu elimu ya
msingi na sekondari kwa kupanga shilingi bilioni 126 tu.
Ø Changamoto nyingine ambayo imekuwapo na imeendelea
kujitokeza katika bajeti ya mwaka huu, ni utegemezi wa bajeti ya maendeleo kwa
wahisani. Uchambuzi unaonesha bado takribani aslimia 50% ya bajeti ya maendeleo
sekta ya elimu inatarajiwa kutoka kwa wahisani.
Ø Changamoto ya mwisho ambayo ni lazima tuiseme, ni
kutokuwepo kwa uwiano kati ya bajeti inayopangwa, fedha ambazo hutolewa na
hazina au wahisani na kiwango ambacho hasa kinatumika katika utekelezaji wa
mipango na bajeti. Kwa miaka mingi wizara, halmashauri na taasiasi zimekuwa
zikitekeleza bajeti pungufu kutokana na kutopatiwa kiwango sahihi kilichopangwa
katika bajeti, na hata kinachotolewa hakitolewi kwa wakati. Hivyo wakati
mijadala ikiendelea juu ya elimu ni muhimu serikali ifikirie upya suala hili na
ikiwezekana kupunguza kiwango cha bajeti kama
utekelezaji utaonekana kuwa na shida. Uchambuzi wa shirika la HakiElimu
unaonesha kuwa kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, matumizi halisi ya
bajeti ya maendeleo ya wizara imekuwa asilimia kati ya 50-65 tu ya bajeti
iliyopangwa.Na hii ndio imekuwa sababu kuu kwa miradi mingi kudorora na
kusababisha sekta ya elimu kubaki na changamoto nyingi na mazingira ya
kufundishia na kujifunzia.
11.
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, hakuna nchi yoyote iliyoendelea hapa duniani
bila kuwekeza kwenye elimu. Malaysia
inajivunia maendeleo yake kwa kuwa iliwekeza kwa vitendo katika elimu. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda
kuwaarifu wananchi wote kwamba, kwa kuwa
Serikali hii ya CCM haina nia ya dhati ya kuboresha elimu yetu kutokana na
kushindwa hata kutekeleza ilani yake kuhusu elimu, Serikali ya Mpya ya UKAWA itakayoingia madarakni baada ya uchaguzi
mkuu wa Oktoba, 2015 itayashughulikia
matatizo yafuatayo katika sekta ya elimu na kuyatafutia ufumbuzi wa kudumu:
i.
Kutokuwa na malengo yakinishi ya
kielimu ya jumla na katika ngazi mbalimbali
ii.
Uhafifu na uduni wa elimu
inayotolewa katika ngazi mbalimbali, na hasa katika ngazi ya msingi na
sekondari yanayodhihirishwa na:
iii.
Kuongezeka kwa idadi ya watu
wasiojua 3K (kusoma, kuandika na kuhesabu)
iv.
Uduni wa shule za sekondari: ni
asilimia nne tu ya shule za sekondari nchini ndizo zinazokidhi vigezo vya chini
kabisa vya hadhi ya sekondari-hizi takribani shule 160 tu kati ya shule za
sekondari zaidi ya 4000 zilizopo nchini.
v.
Uduni wa mazingira ya kufundishia na
kujifunzia katika ngazi mbalimbali za elimu.
vi.
Walimu wasio na motisha na kada ya
ualimu kutelekezwa kwa ujumla
vii.
Kutokuwa na uwiano kati ya
walichojifunza wahitimu na kinachoendelea katika ulimwengu wa kazi, kutokana na
udhaifu wa mitaala na ufundishaji. Matokeo yake: Wahitimu wetu walio wengi
hawaajiriki wala hawawezi kujiajiri.
viii.
Kutokuwa na mfumo thabiti kuhusu
ugharamiaji wa elimu, na hasa elimu ya juu
ix.
Usimamizi dhaifu wa elimu
inayotolewa na taasisi zinazomilikiwa na watu na mashirika yasiyo ya kiserikali
au ya umma. Matokeo yake: tuna mifumo zaidi ya mmoja katika nchi moja
x.
Kutokupewa kipau umbele kwa elimu ya
awali (miaka 3-6) ambayo ndiyo msingi wa kujifunza katika ngazi za baadaye
xi.
Mkanganyiko wa lugha ya elimu
(kufundishia na kujifunzia).
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya kwa niaba ya Kambi Rasmi
ya Upinzani Bungeni, na watanzania wote wanaopenda kuona taifa letu likisonga
mbele kwa kasi ya kumwondoa adui ujinga jambo lililoshindwa kutekelezwa na Serikali ya
CCM, ni UKAWA tu wanaoweza kubadili hali hii kwa kuboresha mfumo wa elimu na
kuwekeza kwa vitendo katika elimu, naomba kuwasilisha.
Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa nawatakia wabunge wote kila la
heri wanapoelekea uraiani baada ya bunge hili kuvunjwa, lakini pia nawatia
ushindi wa kishindo wagombea wote wa udiwani, ubunge na urais watakaopendekezwa
na UKAWA kugombea nafasi hizo, ili Serilali ya awamu ya tano itokane na UKAWA.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuwasilisha.
________________________________
Susan
Anselm Jerome Lyimo (Mb)
MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI
NA WAZIRI KIVULI WA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI
Tarehe 1 Juni, 2015
No comments:
Post a Comment