Thursday, 23 July 2015

Mbowe: Watanzania Mtuvumilie


Mwanza/Dar. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema chama chake kimeshindwa kumtangaza mgombea wake wa urais kama ilivyotarajiwa jana, badala yake kikawaomba Watanzania kutokuwa na haraka, wasiwasi wala mihemko na kuwa muda ukifika kitamtangaza.
Akihutubia mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Magomeni jijini hapa, Mbowe aliwaomba wananchi kuuvumilia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwa sababu viongozi wake wanaendelea na majadiliano na watakapokubaliana watamtangaza mgombea wao.
Awali, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu alisema ilikuwa wamtangaze mgombea urais kama ilivyoripotiwa na gazeti hili, lakini wenzao wa CUF wamewaomba kuwa wanaendelea na vikao vyao vya chama.



 Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), John Mnyika alisema: “Wengi wana hamu ya kutaka kujua mgombea urais wa Chadema, naomba niseme kwamba tumekuja Mwanza kwa mambo mawili, kuja kuwapokea makamanda hawa wawili na kuitokomeza CCM.
“Ukawa itamsimamisha mgombea urais ambaye Oktoba lazima aiondoe CCM madarakani, Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Magdalena Sakaya) ametuomba tena tusubiri hadi tarehe 25 (Jumamosi), kwani watakuwa na kikao cha Baraza Kuu la chama hicho, hivyo tunawasubiri wenzetu.”
Mbowe aliyetumia mkutano huo kuwakabidhi kadi wanachama wapya waliotoka CCM na kujiunga Chadema, Mbunge wa Kahama, James Lembeli na Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya, aliweka msisitizo:
“Muungano wetu wa Ukawa ni wa msingi sana, kuna changamoto, tunaomba wananchi muwe wavumilivu, tuache mihemko ili tufikie uamuzi sahihi.
“Tunaomba mtuvumilie, hatuwezi kumtangaza mgombea wetu kwa sababu tu CCM wametangaza wa kwao, hapana! Tutamtangaza mgombea wetu na nyote mtafurahi,” alisema Mbowe huku akishangaliwa na maelfu ya wananchi.
Alisema, Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi alikuwa ahudhurie mkutano huo lakini kutokana na foleni za Dar es Salaam alishindwa kuwahi ndege na kwamba, viongozi wengine wa CUF na NCCR Mageuzi walialikwa lakini walikuwa na vikao vya vyama vyao.
Mbowe alisema Ukawa ni mpango wa wananchi, siyo wa viongozi na kwamba ulianzishwa Dodoma na viongozi wote wa upinzani na Kundi la Wabunge 201 wa Bunge Maalumu la Katiba walihudhuria, lakini baadhi yao walipenyezewa ‘kitu kidogo’ wakaondoka hivyo kubaki vyama vinne vya siasa.
Udini, ukabila wamkera
Mbowe alionyesha kusikitishwa na kauli alizodai kutolewa na viongozi wa CCM, kumnadi mgombea wao kwa ukabila na kuwataka wananchi kuwakataa wanaotumia mbinu hizo kwani hali hiyo inaweza kusababisha machafuko.
“Nafurahishwa sana na kauli zinazotolewa na viongozi wa CCM, tunampata kiongozi kwa ukabila! Ukawa hatutamchagua mgombea wetu kwa misingi ya ukabila wala udini, huo ni upumbavu,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Msikubali kurudisha ukabila wala udini, hapa uwanjani tupo makabila mengi, Wasukuma mpo! Wahaya, Wachaga, (Ezekiel) Wenje (Mbunge wa Nyamagana) ni Mjaluo yupo hapa.”
Alisema Watanzania wanataka mabadiliko na kwamba hali hiyo imeshuhudiwa wakati wa uandikishaji wa daftari la wapigakura.
Aonya wizi wa kura
Mbowe alisema hawatakuwa na tatizo iwapo ushindi utapatikana kwa njia za haki, lakini hawatakuwa na suluhu iwapo utatumika wizi wa kura kumuingiza mgombea madarakani.
“Hatutapiga magoti na kuomba, kama ushindi utapatikana kwa njia halali hatuna tatizo, lakini tukiona mambo yanakwenda ndivyo sivyo tunasema polisi mtatusamehe, mabomu hayatatosha,” alisema Mbowe.
Lembeli, Bulaya waombewa msamaha
Mbowe alisema Chadema kina maadili yake na kwamba Lembeli na Bulaya waliokuwa CCM wametenda mengi lakini anawaombea msamaha.
“Naomba muwasamehe. Wangapi wanasema tuwasamehe?” alihoji Mbowe huku akiitikiwa kwa sauti, “Woteee”.
Alisema viongozi hao ni miongoni mwa wengi wanaokaribia kutimka CCM na kuwapongeza kwa ujasiri wao makini walioonyesha.
Aahidi kutaifisha viwanja vya CCM
Baada ya kueleza jinsi alivyompigia simu bila mafanikio Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Anthony Diallo kuomba kutumia Uwanja wa CCM Kirumba kwa ajili ya mkutano huo, Mbowe alisema Serikali ya Ukawa ikiingia madarakani itahakikisha viwanja vyote vilivyojengwa na wananchi vinavyohodhiwa na CCM vinarejeshwa kwenye halmashauri.
“Chadema kwa kushirikiana na Ukawa, viwanja vyote vilivyojengwa na wananchi vitarejeshwa kwenye halmashauri ili vitumiwe na wananchi wote,” alisema baada ya baadhi ya wanawake kuzidiwa na kuanguka kutokana na wingi wa watu na ufinyu wa uwanja wa Magomeni.
Wagombea kulishwa yamini
Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa aliwata wagombea ubunge waliopitishwa ambao wana mawazo ya kuuza nafasi zao kwa CCM kujiengua mapema kabla chama hakijawachukulia hatua.
Pia, Dk Slaa alisema chama hicho kitatoa fomu maalumu ambazo zitasainiwa na wagombea ubunge mahakamani ili kiweze kuwachukulia hatua za kinidhamu watakaokwenda kinyume na taratibu za chama hicho.
“Majimbo 157 yamekamilisha leo (jana), sisi Chadema hakuna jimbo ambalo mgombea atapita bila kupingwa kama wanavyofikiri CCM,” alisema Dk Slaa na kuongeza:
“Tutatoa fomu za uteuzi ambazo wote waliopitishwa kugombea ubunge watasainishwa mahakamani, naomba niseme atakayeuza jimbo atashughulikiwa, kama mtu anataka kujitoa ajitoe mapema.”
Dk Slaa alisema miaka 10 iliyopita wananchi waliahidiwa maisha bora kwa kila Mtanzania, lakini yamegeuka na kuwa kinyume, sasa ni maisha magumu kwa kila Mtanzania.
“Waswahili wanasema ukiumwa na nyoka hata jani likikugusa unakimbia, miaka 10 mliahidiwa maisha bora kwa kila Mtanzania, leo ni maisha magumu kwa kila Mtanzania. Cha kwanza tunachokisimamia Chadema ni kurudisha nchi kwa wananchi, CCM wamepoka madaraka ya wananchi na kuyaweka mikononi mwa wachache, tunawaambia mwisho wao ni Oktoba,” alisema Dk Slaa.
Lembeli afunguka
Akizungumza kwenye mkutano huo, Lembeli alisema: “Nakumbuka tarehe 16 nilisali nikiwa kijijini kwetu na mama yangu mzazi, nikamwomba Mungu anitoe nchi ya laana anipeleke nchi ya matumaini.
Tarehe 17 nikafanya uamuzi, sasa nipo uwanjani, naomba niwaambie sijaja Mwanza hivihivi nimekamilika, nilipotoka nimeaga.”
Lembeli aliongeza: “Nimezoea kusema msemo wangu huu, hebu kunja ngumi... koroga... peoples,” umati wa watu uliitikia “Power”.
Kabla hajahutubia, Lembeli alibisha hodi Mwanza kwa kusema: “Hodi…hodi, aliitikiwa kwa sauti na umati uliohudhuria: “Karibu baba, karibu.”
Bulaya ampa salamu Wasira
Akihutubia baada ya kukabidhiwa kadi ya uanachama, Buyala alianza kwa kuwauliza wananchi: “Nikamtoe? Nauliza, nikamtoe? Nikamtoe nani?” wananchi walijibu kwa sauti kubwa: “Wasira... kamtoe Wasira.”
Bulaya alisema ni bora kama Waziri wa Chakula, Kilimo na Ushirika, Stephen Wasira anamsikia akaondoka kama alivyomshauri Makongoro Nyerere.
“Makongoro Nyerere alisema, awamu ya kwanza upo, awamu ya pili upo, ya tatu upo ya nne upo ya tano mwisho wake umefika sasa,” alisema Bulaya.
Alisema kwa Mkoa wa Mara yupo mwenyekiti wake, Vicent Nyerere ambaye atafanya naye kazi kwa karibu na kwamba yeye na wenzake wa Chadema ni muziki mnene na jeshi kubwa.
Lissu na kabila la CCM
Akihutubia kwenye mkutano huo, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu aliwalinganisha, Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Andrew Chenge na Spika Anne Makinda kwamba hawana tofauti na mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli, kwa sababu wote ni kabila moja la CCM.
“Nimefanya mikutano mingi, kila mahala nilipokwenda nilikuwa naambiwa Dk Magufuli kabila lake ni Msukuma, wengine Msubi na wapo waliosema Mzinza, mimi naomba niwaambie kwamba kabila moja la CCM ndilo la Dk Magufuli,” alisema Lissu.
Alisema Dk Magufuli ndiye aliyeuza nyumba za Serikali nchi nzima, kauli ambayo ilitiliwa mkazo na Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari ambaye alisema watumishi wa umma wanaishi kwenye nyumba za vichochoroni kutokana na Dk Magufuli kuuza nyumba za Serikali.
Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini wa Chadema, Arcado Ntagazwa ambaye aliwahi kuwa waziri na naibu waziri kwa miaka 15 alisema: “Safari hii kwa Chadema na washirika wao wa Ukawa ni moja kwa moja Ikulu.
Goli la mkono laibuka
Ntagazwa alisema: “Mambo ya kusema goli la mkono, watambue kwamba Oktoba ndiyo mwisho wa ufisadi,”
Kauli hiyo iliungwa mkono na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee ambaye alisema mwaka huu goli la mkono litawageukia wao... “Wakijifanya wao ni watoto wa kihuni makamanda wa Chadema ni wahuni zaidi yao.”
Kuhusu kucheza rafu, Mwalimu alisema wanaotarajia kucheza rafu kwenye uchaguzi mkuu ni wazi kwamba wameshindwa kucheza uwanjani.
“CCM kutangaza kushinda hata kwa goli la mkono ni wazi kwamba wameshindwa kucheza uwanjani sasa sisi tutawafuata hukohuko nje ya uwanja na tutawabana,” alisema Mwalimu.
Wenje, Kiwia watamba
Mbunge wa Nyamagana, Ezekia Wenje na Highness Kiwia, walisema kwa sasa wapo likizo ya miezi miwili na wanatarajia kuapishwa tena kuwa wabunge baada ya uchaguzi.
Kiwia alisema: “Mimi ndiye rais wa Jamhuri ya watu wa Ilemela, sina shaka tumemaliza kura za maoni sasa nasubiri tena kuwa Mbunge wa Ilemela.”
Akihutubia, Nyerere ambaye pia ni Mbunge wa Musoma Mjini, alisema kazi inaendelea na kinachofanyika sasa ni kuhakikisha CCM inaondoka madarakani Oktoba.
Leo viongozi hao wa Chadema watakuwa na mkutano mwingine mjini Mbeya na baadaye Arusha na Jumatatu ni Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment