Monday 31 August 2015

LOWASSA AUNGURUMA IRINGA

Mgombea Urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa amesema amechoshwa na manyanyaso wanayoendelea kuyapata wakulima hapa nchi kwa kukopwa mazao yao na kutozwa ushuru na serilkali bila ya wao kupata faida yoyote.

Lowassa alisema punde atakapochaguliwa kuongaza nchi kitu kikubwa atakachokifanya kuwasaidia wakulima ni kufuta ushuru wote wa mazao kuhakikisha wakulima wananufaika na jasho wanalolitoa wakati wa kilimo.

Lowasa ameyasema hayo leo wilayani Mufindi alipofanya mkutano wa hadhara wa kampeni katika Uwanja wa Shule ya Msingi Wambi, mjini Mafinga.

Lowassa alisema watu wamekuwa wakizungumza kuwa CCM ni wezi wa kura kwasababu ni wajanja sana katika kufanya michezo michafu katika chaguzi na maneno hayo si yakuyabeza wala kuyafumbia macho.

“Mimi nataka kila mtu akihifazi vizuri kichinjio chake (kadi ya kupigia kura) na siku ya kupiga kura ikifika nawaomba wanawake na wanaume wajitokeze kwenda kupiga kura ila wakina baba nawaomba mkishapiga kura fanyeni kazi ya kuzilinda kura zenu” alisema Lowassa

Katika mkutano huo, waziri wa zamani wa Elimu, Joseph Mungai alipanda jukwaani na kumnadi Mgombea Ubunge wa Jimbo la Mafinga Mjini kupitia Chadema, William Mungai ambaye ni mtoto wake.

Mungai aliwahi kuwa mbunge kwa miaka 35 kupitia CCM na aliweza kuteuliwa nafasi mbalimbali za uwaziri ikiwamo Wizara ya Kilimo, Mambo ya Ndani na Wizara ya Elimu.

Mungai alisema wananchi wa jimbo hilo wanatakiwa kumchagua William Mungai kwa sababu mbunge aliyemaliza muda wake katika jimbo hilo hakuweza kuongoza kama alivyofanya yeye.

 Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungani wa Tanzania katika mwamvuli wa UKAWA kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mh. Edward Lowassa akimnadi Mgombea Ubunge wa Jimbo la Mafinga Mjini, William Joseph Mungai, wakati wa Mkutano wa Kampeni, uliofanyika kwenye Uwanja wa Wambi, Mafinga Mjini, Mkoani Iringa leo Agosti 30, 2015.
 Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungani wa Tanzania katika mwamvuli wa UKAWA kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mh. Edward Lowassa akimnadi Mgombea Ubunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa wakati wa Mkutano wa Kampeni, uliofanyika kwenye Uwanja wa Sabasaba, Mkoani Iringa leo Agosti 30, 2015.Picha na Othman Michuzi, Iringa.
 Waziri wa zamani wa Elimu, Mh. Joseph Mungai akihutubia kwenye Mkutano wa Kampeni za Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungani wa Tanzania katika mwamvuli wa UKAWA kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mh. Edward Lowassa, uliofanyika kwenye Uwanja wa Wambi, Mafinga Mjini, Mkoani Iringa leo Agosti 30, 2015.
 Waziri Mkuu wa Mstaafu, Mh. Fredrick Sumaye akihutubia kwenye Mkutano wa Kampeni za Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungani wa Tanzania katika mwamvuli wa UKAWA kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mh. Edward Lowassa, uliofanyika kwenye Uwanja wa Wambi, Mafinga Mjini, Mkoani Iringa leo Agosti 30, 2015
 Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungani wa Tanzania katika mwamvuli wa UKAWA kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mh. Edward Lowassa akimsalimia kijana mwenye ulemavu (jina lake hakupatikana kwa haraka) aliyehudhulia Mkutano wa Kampeni ya Mgombea huyo, uliofanyika kwenye Uwanja wa Sabasaba, Iringa Mjini, leo Agosti 30, 2015.Picha na Othman Michuzi, Iringa.

 Umati wa Wakazi wa Mji wa Iringa Mjini ukiwa umefurika kwa wingi kwenye Uwanja wa Sabasaba, kulikofanyika Mkutano wa Kampeni za Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungani wa Tanzania katika mwamvuli wa UKAWA kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mh. Edward Lowassa, leo Agosti 30, 2015




HOTUBA YA MGOMBEA URAIS KUPITIA CHAMA CHA CHADEMA NA UKAWA MH. EDWARD NGOYAI LOWASSA YA KUZINDUA ILANI NA KAMPENI YA UCHAGUZI MKUU


Jangwani-Dar-es-Salaam, 29 AGOSTI 2015

Ndugu Wana Dar es salaam na Watanzania wenzangu
Leo ni siku ya kihistoria. Baada ya miaka ishirini na tano tangu mfumo wa vyama vingi urejeshwe, vyama vya upinzani wa CHADEMA, CUF, NCCR na NLD umeungana chini ya Umoja wa Katiba ya Wananchi kupigania uchaguzi mkuu wa mwaka huu na kuwa na mgombea mmoja katika ngazi zote.
Miaka zaidi ya hamsini ya utawala wa serikali za CCM na waasisi wake, umekuwa utawala wa wachache walio hodhi madaraka na mali za nchi.
Leo tunaanza safari ya uhakika ya kuleta mabadiliko ya kweli nchini.
Mabadiliko yaletayo neema na kujenga upya mfumo wa uchumi, haki na sheria nchini.
Mabadiliko ya kuimarisha huduma za jamii kama elimu, afya, maji na makazi.
Mabadiliko ya kuondoa umaskini.
Mabadiliko tunayatoahidi ni mabadiliko ya kurejesha matumaini kwa Watanzania kwa kubadili hali zao za maisha.
Kila mwaka hali na ubora wa maisha ya Watanzania imeshuka wakati tunaambiwa kuwa pato laTaifa linakuwa.
Lakini Watanzania wanachotaka siyo takwimu bali kuona kipato chao kinakua, shule, hospitali na barabara bora zinajengwa.
Wanataka kupata maji safi na salama ya kunywa. Wanataka makazi bora.
CHADEMA na UKAWA, tuna dhamira ya kuleta mabadiliko ya kweli ili kuona azma ya Watanzania tangu uhuru ya kuondoa umaskini, maradhi,na ujinga inahitimishwa.
Ili tufanye hivyo tuahitaji tufanye mabadiliko ya fikra, uongozi, sera na utendaji.
Leo Tanzania inakabiliwa na changamoto nyingi za ki-uchumi, kisiasa na kijamii. Changamoto hizi ni matokeo ya sera za utawala wa Chama kimoja wa miaka hamsini. Sote ni wahanga wa siasa na sera hizi.
Miaka Hamsini ya CCM imetosha. Tunataka mabadiliko na siyo ahadi zile zile kila mwaka
Tusidanganyike, CCM hawana jipya
Chagueni UKAWA wenye dira ya kubadili maisha ya wananchi.
Mimi ninauchukia umaskini na mimesimamia maendeleo kwa vitendo. Nilipokuwa Waziri Mkuu nilijaribu kubadili hali hii. Nilisimamia ujenzi wa shule za kata, Chuo Kikuu cha Dodoma. Nilihakikisha mikataba mibovu ya maji inavunjwa na sasa wananchi wa kanda ya ziwa wanapata maji safi.

Ndugu watanzania
CCM wanauliza tuna mpango gani wa kumaliza umaskini. Sisi hatuahidi tu. Tutatenda.
Ilani yetu ni dira ya kuondoa umaskini kwa mikakati sahihi na siyo nadharia.
Mkakati wa kuondoa umaskini si wa sekta kwa sekta bali wa sekta zote kwa pamoja. Ni ujumla wa utendaji na utekelezaji wa sera za kila sekta utakao leta maendeleo.
Mkakati wangu na UKAWA wa kuondoa umaskini utakuwa na nguzo tano:-
Kupunguza matumizi ya serikali na mashirika yake na kuimarisha utendaji na uwajibikaji.
Kukuza pato la serikali kwa kudhibiti ukwepaji na misamaha ya kodi holela na kuhakikisha nchi inawekeza katika sekta muhimu na inapata gawio halisia kutoka wawekezaji
Kukuza uchumi kwa sera na sheria endelevu ikiwa ni pamoja na kukuza biashara na uwekezaji hasa katika sekta za madini, kilimo, viwanda, ufugaji na uvuvi na kuondoa kodi kwa wanyonge.
Kuimarisha huduma za umma kama elimu, afya, maji na makazi, na mazingira
Kuimarisha utawala bora na mfumo wa haki na sheria chini ya Katiba ya Wananchi.
Chini ya misingi hii na ili kufanikisha mkakati wa kuondoa umaskini, serikali yangu itafanya yafuatayo:-

ELIMU BORA KWA KILA MTANZANIA

Nimelisema hili huko nyuma. Nalisema tena leo. Elimu kwanza, Elimu kwanza, Elimu kwanza.

Kwa hiyo mkakati wetu wa msingi utakuwa kutoa Elimu itatayogharamiwa na serikali kwa kila Mtanzania kutoka elimu ya msingi hadi Chuo Kikuu na pia:-
Kuimarisha elimu ya teknolojia, ustadi na ufundi inayojenga uwezo wa kujiajiri na ushindani katika soko la ajira.
Ujenzi na uimarishaji wa miundombinu ya elimu ikiwa ni pamoja na shule za Kata.
Kusimamia ubora wa viwango vya elimu kote nchini.
Kuimarisha taaluma na mitaala katika mashule.
Kuondoa utoro darasani, na kuboresha afya za wanafunzi.
Kuboresha maslahi na vitendea kazi kwa walimu ikiwa ni pamoja na nyumba, posho ya kufundishia, usafiri na zana za teknolojia.
Kufuta michango ya maabara ya shule za kata



AFYA
Afya na tiba ya kila Mtanzania itagharamiwa kupitia bima za gharama nafuu na mifuko ya hifadhi ya jamii
Tutaimarisha afya ya msingi pamoja na kinga kupunguza gharama za tiba.
Serikali itahakikisha kuna uwiano na upatikanaji wa watumishi wa afya katika kada mbalimbali ili kuleta tija na huduma stahiki.
Itaimarisha miundombinu ya afya pamoja na kujenga hospitali za kisasa ili kusogeza huduma za afya karibu na jamii na pia kuepukana na tiba za nje ya nchi.
Tutarejea kwa lengo la kuboresha maslahi na vitendea kazi katika sekta ya Afya ikiwa ni pamoja na nyumba na usafiri.
Tutathibiti ongezeko la gharama za huduma za afya bila kuathiri uendeshaji wa watoaji huduma za afya kama vile serikali na hospitali za sekta binafsi.



ARDHI, MAJI NA KILIMO
Tutaimarisha mfumo wa umiliki wa ardhi kwa Watanzania na kudhibiti migogoro ya ardhi hasa kati ya wakulima na wafugaji.
Tutapima ardhi yote ya Tanzania na kumilikisha vijiji na wakulima kwa hati za serikali ili kuipa thamani.
Tutaleta mapinduzi ya kilimo kwa kuimarisha elimu, ufundi na teknolojia ya kisasa na kumkomboa mkulima kutoka jembe la mkono.
Tutasimamia kilimo, ufugaji na uvuvi wa kisasa na kuunganisha sekta hizo na ya viwanda.
Kuhakikisha kuwa wananchi wanatunza na kulinda vyanzo vya maji.
Tutakuza kilimo cha umwagiliaji kwa kuwapa wakulima elimu na mikopo ya riba nafuu ya kuvuna maji na kujenga miundombinu husika.
Tutaweka mazingira rafiki yatakayomhakikishia kwa kila Mtanzania kupata maji safi na salama. Kumaliza kero za maji nchini kutamkomboa mwanamke kutokana na adha ya kuchota maji kwa kichwa
Nitafuta kodi zote za mazao na mifugo kwa wakulima na wafugaji.
Tutasimamia kilimo cha biashara kinachozingatia maslahi ya nchi na ya Watanzania.
Tutaanzisha programu maalum ya kufufua mazao asilia ya Tanzania hususan mkonge.
Tutaanzisha Benki ya Maendelo ya Ufugaji na Uvuvi.



MIUNDOMBINU
Tutaboresha bandari zilizopo na kujenga mpya kama vitega uchumi vya Taifa ili kurejesha biashara tulizopoteza kwa bandari za nchi jirani.
Tutajenga barabara nchini kwa kuzingatia ubora hasa zile za vijijini.
Tutajenga reli ya kati kwa viwango vya kisasa
Tutajenga shirika la Ndege la Taifa linalojiendesha kwa misingi ya faida.
Tutajenga miundombinu ya kisasa na kuondosha misongamano ya magari hasa katika majiji ya Dar es salaam, Mwanza, Mbeya na Arusha
Tutaimarisha uzalishaji na usambazaji wa umeme vijijini ili kufikia zaidi ya asili mia sabini na tano ya Watanzania
VIWANDA
Tutaimarisha sekta ya viwanda kuwa mhimili wa uchumi kwa uzalishaji wa bidhaa na ajira endelevu
Tutajenga viwanda vipya vya kusindika mazao ya kilimo, uvuvi na ufugaji.
Tutahakikisha kuwa ndani ya miaka mitano mali ghafi zote za Tanzania zinasindikwa kabla ya kusafirishwa nje ili kuongeza mapato na ajira ya mamilioni ya vijana.
Tutaanzisha Benki ya Ukuzaji wa Viwanda



UCHUMI
Tutabadili mfumo wa Uchumi wa nchi ili kuhakikisha kuwa mfumo wa uchumi wa Tanzania unakuwa ni wa soko-kijamii ambapo nguvu za soko zitatumikia jamii kwa serikali kuweka uwiano wa mapato unaohakikisha huduma za kijamii zinapatikana kwa ufanisi.
Tutalinda sekta binafsi na bidhaa za ndani kwa kuwapa Watanzania upendeleo wa maksudi kwa kipindi cha mpito ili waimarike na waweze kuhimili ushindani. Tutawapa wafanyabiashara wetu upendeleo katika manunuzi ya serikali na kuwajengea mazingira mazuri ya biashara na kodi endelevu.
Tutawawezesha Watanzania kupata mitaji ya biashara kwa masharti nafuu kabisa.
Tutavutia uwekezaji na wawekezaji wenye tija. Kuweka udhibiti wa wahamiaji wasioleta tija wala maslahi kwa Taifa.
Tutaimarisha sera ya ubia baina ya Serikali na Sekta binafsi kwenye maeneo muhimu ya kiuchumi na kibiashara. Pia, kuwawezesha Watanzania kuwekeza kwa njia ya ubia na wawekezaji wenye mitaji mikubwa bila kujali wanapotoka.
Tutaimarisha usimamizi kwa kubadilisha mfumo wa Vyama vya Ushirika nchini ili utokane na uendeshwe na wakulima wenyewe ikiwa na pamoja na kuwawezesha kuboresha makazi kwa mpango wa kushirikiana kujenga nyumba bora
Tutaanzisha na kuwezesha uanzishaji wa viwanda vidogovidogo vinavyotoa ajira kwa wingi kwa kuvihusisha na vyuo vya ufundi na benki maalum kwa lengo hilo.

AJIRA
Tutasimamia swala la ajira hasa kwa vijana kwa kukuza elimu ya ufundi ili waweze kujiajiri
Tutazipa kipaumbele sekta zinazozalisha ajira kwa wingi hasa za viwanda, kilimo, ufugaji, uvuvi na utalii na kuzipa unafuu wa kodi ili zikue kwa haraka.
Tutawapa wawekezaji wakubwa katika sekta hizi upendeleo maalum na viwango vya kodi nafuu.

NISHATI NA MADINI
Serikali itashiriki kikamilifu katika uzalishaji wa nishati
Itatengeneza mazingara mazuri ya kisera yatakayovutia na kuwezesha ushiriki wa Watanzania na ubia kati yao na wageni.
Serikali yangu itaupa uzalishaji mkubwa wa umeme wa maji kipaumbele namba moja, umeme wa makaa ya mawe kipaumbele namba mbili, umeme wa gesi asilia kipaumbele namba tatu na umeme wa urana kipaumbele namba nne.
Serikali itatoa vipaumbele muhimu kwenye usambazaji wa huduma kubwa ya umeme sehemu za uzalishaji uliyolenga masoko ya ndani, ya nchi jirani na ya nchi za kigeni.
Itapitia upya mikataba yote mikubwa ya nishati na madini ili kubaini iliyo mibovu na kuifanyia maboresho.
Serikali yangu itatumia sehemu ya hisa zake kwenye raslimali kubwa ya gesi asilia iliyopatikana hapa nchini kama rehani kwenye kujichukulia mikopo kwa ajili ya ujenzi wa miundo mbinu ya mabomba ya gesi.
Serikali itatoza kodi na ada ndogo zaidi kwa wazawa wenye ubia kati yao na wageni kuliko zitakazotozwa kwa wageni wasiowekeza kwa kushirikisha wazawa.


Serikali itasitisha utoaji wa misamaha ya kodi isiyo lazima kwenye sekta ya madini, na badala yake itawekeza kwenye kuongeza thamani ya raslimali zake za madini.
Tutakuza nishati mbadala kutamkomboa mwanamke kutokana na adha ya kukata kuni



MALIASILI NA UTALII
Tutasimamia uvunaji na matumizi ya rasilimali za Taifa kwa manufaa ya kila Mtanzania wa kizazi hiki na kijacho
Tutapiga vita ujangiri na kuimarisha utunzanji wa hifadhi za taifa na mazingira
Tutachochea ujenzi wa miundombinu ya utalii nchini ikiwa ni pamoja na ujenzi wa mahoteli na kuimarisha mafunzo
Tutaongeza idadi ya watalii kufikia milion mbili ifikapo 2020.


UTAWALA BORA, ULINZI WA NCHI NA USALAMA WA RAIA
Tutasimamia Katiba mpya inayolinda haki za msingi za wananchi na kuweka bayana mipaka ya madaraka ya serikali na viongozi, Bunge na Mahakama.
Tutasimamia haki za raia na kuangalia upya sheria kandamizi ili wananchi kama Masheik wa Zanzibar hawasoti jela kwa sababu za kisiasa.
Tutaimarisha mafunzo ya vyombo ya Polisi hasa wapelelezi na waongoza mashtaka ili wapate uwezo wa kusimamia utoaji wa haki.
Tutavipa vyombo vyote vya ulinzi na usalama nyenzo na kuboresha mazingira yao ya kazi na maslahi

UZALENDO, UTENDAJI NA UWAJIBIKAJI
Tutajenga uzalendo ili kila Mtanzania aweze kutathmini mchango wake kwa taifa kila siku
Tutaimarisha nidhamu, utendaji na uwajibikaji katika Sekta ya Umma
Tutaimarisha mchango wa Wataalam wetu, wanawake na vijana katika kusimamia uchumi na kuwajengea mazingira stahiki ya kazi pamoja na mafao.
Tutapiga vita rushwa na ubadhirifu katika sekta ya Umma na binafsi
Tutadhibiti na kupunguza matumizi ya serikali ikiwa ni pamoja na kufuta safari za watumishi serikalini zisizokuwa muhimu pamoja na zile za Rais na kupiga marufuku matumizi ya mashangingi serikalini.
Tutadhibiti deni la Taifa kwa kuanza na ukaguzi wa madeni ya serikali ili kuhakiki jinsi yalivyotumika
Tutaimarisha uwazi na kuondoa usiri katika shughuli za serikali na kuweka bayana mikataba yote ya nchi ikiwa ni pamoja na ile ya mafuta, madini na gesi asilia

KUKUZA PATO LA SERIKALI
Tutadhibiti mapato kutokana na raslimali kwa kupitia upya viwango vya mirabaha kutokana na madini na gesi asilia ili kuhakikisha kuwa Tanzania inapata gawio stahiki.
Serikali itaanzisha Wizara maalum itakayosimamia nishati ya gesi na mafuta.
Tutaimarisha ofisi ya Msajili wa Hazina ili kusimamia vema uwekezaji wa Serikali katika mashirika na mapato yake.
Tutahakikisha kuwa mashirika ya umma yanaendeshwa kwa misingi ya faida na uadilifu.
Tutadhibiti ukwepaji kodi za ushuru wa forodha na kupiga marufuku misamaha ya kodi holela ili kuokoa mabilioni ya fedha yanayopotea kila wiki.
Sambamba na hilo tutarahisisha utaratibu wa kulipa kodi ili kuondoa kero na mazingira ya rushwa. Kwa kudhibiti makusanyo ya kodi tutakusanya fedha za kugharimia huduma za msingi kama afya na elimu kikamilifu.

KUIMARISHA MUUNGANO
Tutaimarisha umoja, usalama na udugu wa Watanzania na Muungano kwa misingi ya haki na usawa

WANAWAKE, WATOTO NA WAZEE
Wanawake watapewa fursa na haki sawa katika elimu na uchumi ili waweze bila kuwezeshwa.
Tutahakikisha wazazi wanapata fursa ya kuwa walezi na wafanyakazi kwa kuongeza urefu wa likizo ya uzazi
Tutaimarisha elimu ya watoto hasa wasichana na kukuza fursa zao na kukomesha ndoa za watoto wadogo.
Tutaongeza uwakilishi wa akina mama katika ngazi zote serikalini na mashirika yake kufikia asili mia hamsini ifikapo 2020.
Wazee na wasiojiweza watapewa posho ya kujikimu inayokidhi mahitaji ya msingi itakayowawezesha kuishi kwa heshima na kulinda utu wao ndani ya familia na jamii zao.
SANAA, UTAMADUNI NA MICHEZO
Tutaendeleza na kuwezesha vipaji vya sanaa na michezo
Tutarudisha viwanja vya michezo vilivyovamiwa
Tutafuta kodi zote za vifaa vya michezo.
Tutadhibiti viwango na maadili ya bidhaa za nje zinazoingizwa nchini na kuzitoza kodi halisia
Tutajenga taasisi na vyuo vya kukuza michezo ili kuhakikisha kuwa ndani ya miaka mitano Tanzania inashiriki kwa ushindi katika mashindano ya kimataifa ya soka na riadha
Tutalinda Hakimiliki za sanaa nchini
Tutafuta kodi za sanaa kwa wasanii chipukizi ili kuwapa muda kwa kujijenga.

SERA YA MAMBO YA NJE YENYE TIJA KWA TAIFA
Tutakuza ushirikiano wa Kimataifa wenye tija na Ujirani mwema.
Tutatetea haki za binadamu, usawa wa nchi na kuimarisha ushiriki wa Tanzania katika diplomasia ya kimataifa.
Tutakuza umoja na ushirikiano wa Umoja wa Afrika, Jumuia ya Afrika Mashariki, SADC na Umoja wa Mataifa.
Tutaimarisha Umoja wa Mataifa ikiwa ni pamoja na kudai mabadiliko ya mfumo ili kuleta usawa wa nchi shiriki.

Ndugu Watanzania

Naomba nimalizie kwa kusema yafuatayo
Natambua kuwa uongozi ni dhamana. Mkinichagua nitaienzi dhamana hiyo kwa utendaji uliotukuka.
Nawaahidi Watanzania kuwa kwa uwezo, akili, uzoefu na nguvu zangu zote nitawatumikia. Nawaomba nanyi mniahidi jasho lenu na uwezo wenu wote ili kwa pamoja tuvuke. Tutajikomboa toka utawala wa CCM unaodumaza uchumi na maendeleo. Tutaanza safari ya uhakika kuondoa umaskini.
Mabadiliko pia ni kuthamini utu na kukataa hadaa ya hongo ili kuuza haki yako ya kuchagua. Msikubali rubuni za uchaguzi kwa kupewa pesa au vitu. Rushwa ya uchaguzi ndiyo sera ya CCM. Ukikubali basi umeuza pia haki na sauti yako ya kuwalalamikia walio madarakani. Imetosha. Tukatae. Tulinde utu na haki zetu. Tuchague mabadiliko.
Mabadiliko ni fikra. Ni kufikiri na kutenda tofauti. Hatuwezi kuendelea kufikiri na kutenda kama kwamba hatuna dharura ya maendeleo. Kwanza tuanze kwa kufanya mabadiliko na tujiamini kuwa sisi kama Taifa tunaweza. Tunaweza kujitegemea na kuleta maendeleo yetu wenyewe bila kutegemea wafadhili. Hii si ndoto. Nchi nyingi zimefanikiwa kuondoa umaskini katika kizazi kimoja. Tujifunze kutoka kwao.
Tuwe taifa linalotumia raslimali zake kujiendeleza na siyo kuwanufaisha wageni na kuwafanya Watanzania watwana katika nchi yao. Inabidi tuache kuwa taifa ombaomba. Tuache kuukubali na kuvaa umaskini kama joho la fahari.
Mabadiliko ya kweli hayawezi kuletwa na CCM. Tusitegemee kuwa leo wana jipya. Ndiyo maana ahadi walizotoa miaka thelathini iliyopita ndizo wametoa juzi. Tukatae hadaa. Miaka hamsini ya CCM imetosha.
Tunaamani kwamba tutashinda kwa sababu Watanzania mpo nyuma yetu. Watanzania mmeamua kuleta mabadiliko. Kura yako ndiyo itakayokuwa mkombozi wako. Hakikisha unapiga na kuilinda kura yako. Wakati wa mabadiliko ni sasa.

TASWIRA: MKUTANO WA UFUNGUZI WA KAMPENI ZA UKAWA








Thursday 27 August 2015

RATIBA ya Kampeni za Mgombea Urais wa CHADEMA/UKAWA na mgombea mwenza






Mbowe akata rufaa mahakama kuu dhidi ya hukumu yake




Uchaguzi Mkuu 2015: Serikali Yapiga Marufuku Kutumia Helikopta Wakati wa Kampeni Bila Kibali

  1. UTANGULIZI
    1. Tangazo hili linatolewa kwa lengo la kutoa mwongozo kwa watoa huduma za helikopta, marubani wake na umma kwa ujumla kuhusiana na hatua za kiusalama zinazopaswa kuzingatiwa inapolazimika kutoa huduma ya usafiri wa helikopta hapa nchini, hususan, maeneo ya mbali (vijijini) ambapo huduma za uongozaji ndege hazipo au sio maeneo maalum yaliyotengwa kwa ajili ya helikopta kutua (mahsusi kwa helikopta au viwanja vya ndege kwa ujumla). Tangazo hili limetolewa baada ya Mamlaka kugundua kwamba kumekuwa na matumizi mabaya ya huduma hizi kinyume na kanuni za usafiri wa anga nchini na weledi unaozingatia taratibu za kitaaalamu na miongozo katika usafiri wa anga.
      .
    2. Mamlaka inatambua kwamba matumizi ya helikopta wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 yanatarajiwa kuongezeka na kuna uwezekano wa kuleta athari za kiusalama kwa maisha ya watu na mali pamoja na watumiaji wa vyombo hivi. Pia vitendo vya kuning’iniza vitu kama mabango ya matangazo mbalimbali kwa kutumia ndege (helikopta ikiwemo) yanaweza kuleta hatari endapo sheria na taratibu zinazohusiana na matumizi hayo hazitazingatiwa.
    3. Tangazo hili linatolewa kwa mamlaka aliyopewa Mkurugenzi Mkuu chini ya Sheria Namba 80 ya Usafiri wa Anga na kanuni zake zinazohusiana na masuala ya usafiri wa anga nchini zilizowekwa kwa lengo, hususan, kuhakikisha usalama katika matumizi ya vyombo vya usafiri wa anga sambamba na kulinda usalama wa umma na mali wakati wa matumizi ya vyombo husika.
    4. Watoa huduma za usafiri wa helikopta au ndege na marubani wake wanaokodishwa kutoa huduma wakati wa kampeni, na mtu yeyote anayetarajiwa kutumia huduma hiyo wanakumbushwa kuhakikisha wanazingatia kanuni za usafiri wa anga na ikibidi kuomba kibali kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania. Kanuni zinapatikana kupitia tovuti yetu kwa anuani ya:www.tcaa.go.tz; na endapo utahitaji maelezo ya ziada au miongozo zaidi usisite kuwasiliana na Mamlaka.
  2. CHETI CHA NDEGE KWA USALAMA WA KURUKA – AIRWORTHINESS CERTIFICATE
    1. Helikopta yeyote itakayotoa huduma katika kampeni za kisiasa lazima iwe ina cheti halisi cha usalama wa kuruka kilichotolewa na mamlaka husika ya helikopta ilikosajiliwa. Kwa hapa nchini cheti hicho ni lazima kiwe kimetolewa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga. Na cheti hicho ni lazima kiwe kimetolewa kwa ajili ya helikopta yenye usajili na mahsusi kwa kazi ya kubeba abiria ambayo inaweza kutumika kwa shughuli nyingine zozote. Kwa tangazo hili helikopta nyingine yeyote ile isiyokuwa na sifa hiyo haiwezi kutumika kufanya biashara ya usafiri wa abiria katika kampeni.
    2. Endapo helikopta itakuwa ina usajili wa nje ya Tanzania, mtu anayetarajia kuitumia hapa nchini ni lazima apate kibali cha kuiingiza nchini na kuitumia kwa usajili wa nchi iliyotoka kama ilivyoainishwa katika Waraka wa Mamlaka unaoainisha taarifa za usafiri wa anga – Aeronautical Information Circular (AIC 08/09). Hakikisha unapoomba kibali uwe umekidhi vigezo vya waraka huu ikiwa ni pamoja na kuwasilisha nakala za nyaraka zinazopaswa kuwasilishwa zikiwemo cheti cha usajili wa ndege, cheti cha ndege kwa usalama wa kuruka, cheti cha leseni za radio za ndege, cheti cha bima, makubaliano/mkataba wa kukodisha ndege hiyo, utaratibu wa kufanya matengenezo ya ndege hiyo, leseni za marubani, na ushahidi wa karibuni wa matengenezo ya ndege hiyo.
  3. TARATIBU ZA USALAMA WA UENDESHAJI
    1. Mahitaji ya jumla ya kiuendeshaji

      Matakwa ya marubani na uendeshaji unatakiwa kufuata maelekezo husika yaliyomo kwenye Kanuni inayohusiana na uendeshaji, yaani, The Civil Aviation (Operation of Aircraft) Regulations. Rubani Mkuu anawajibika kuhakikisha kwamba vituo vya Mamlaka vya kuongoza ndege vinavyohusika katika eneo atakalokuwepo au kwa utaratibu wa uongozaji ndege, wanakuwa na taarifa za mpango wake mzima wa safari husika kwa siku au wakati husika.

      Njia itakayotumiwa na rubani izingatie matakwa ya kuepuka kuruka chini ya kiwango cha umbali unaotakiwa hasa katika maeneo yenye watu wengi yakiwemo maeneo yaliyopangwa kufanyika kwa mikutano husika.

      Tahadhari ni lazima zichukuliwe wakati wa kuelekea kutua, kutua kwenyewe na hata wakati wa kuondoka, hasa ikizingatiwa kuwa kuna uwezekano wa wananchi kuikimbilia helikopta au eneo la utuaji. Katika hali yeyote ile rubani hapaswi kutumia chombo chake kukusanya wananchi kwa ajili ya mkutano au kuitumia kwa utaratibu wowote mwingine kinyume na matakwa ya kiurukaji kwa ndege husika.
    2. Usalama wa eneo la kutua na kuruka

      Maeneo yote yatakayotumika kwa ajili ya kutua ama kuruka ni lazima yafahamike mapema. Maeneo ya kuruka ama kutua ni lazima yawe mbali na eneo mkutano utakapofanyika ili kuweza kutoa eneo salama kwa ajili ya kuruka ama kutua kutoka katika mikusanyiko ya watu.

      Maeneo ambayo yatatambuliwa kama ni ya kuruka ama kutua hasa yale ambayo hayajatambulika kisheria kwa kufanyia shughuli hiyo ni lazima yawekewe alama maalum na uzio ili kuzuia watu wasiohusika kusogelea eneo hilo.

      Eneo husika ni lazima lilindwe; rubani mkuu ahakikishe helikopta itakayokuwa imetua eneo hilo inalindwa dhidi ya uvamizi kutoka kwa watu wasiohusika. Hatua maalum za kiulinzi ni vyema kuchukuliwa endapo kutakuwa na ulazima wa chombo hicho kulala katika eneo husika usiku mzima. Kila wakati rubani anapotaka kuruka ni vyema ahakikishe amekagua chombo chake kwa mujibu wa taratibu zinazohusika kwa umakini kabla ya kuanza safari.
    3. Usiamizi wa Chombo kikiwa ardhini na usalama kwa umma

      Mtu mwenye wajibu wa usimamizi wa chombo kikiwa ardhini lazima awe ni mwenye mafunzo ya kutosha na awe anajua madhara yanayoweza kusababishwa na mapanga ya helikopta yanapozunguka. Kwa marejeo zaidi kuhusiaha na hilo tafadhali zingatia yaliyomo kwenye Waraka wa Mamlaka AIC33/2000 unaoelezea masuala ya madhara yanayoweza kusababishwa na mapanga ya helikopta yanayozunguka.

      Ni wajibu wa Rubani mkuu na mhusika aliyekodisha helikopta kuhakikisha wananchi wanakuwa salama na mbali na helikopta. Matumizi ya kizembe na yasiyo ya kiweledi ya helikopta yatakayohatarisha usalama wa wananchi yatachukuliwa kama ukiukwaji wa kanuni za usafiri wa anga na Mamlaka itawachukulia hatua kama ilivyoanishwa kwenye kanuni hizo.
    4. Kuchukua na kuangusha vitu ardhini na kupeperusha mabango angani

      Huduma hizi zinaweza kufanywa na helikopta na hata ndege zingine za kawaida. Kabla ya kufanya shughuli za namna hiyo, mmiliki wa chombo ni lazima ahakikishe anakidhi vigezo vya Kanuni za Usafiri wa Anga kwa huduma hizi, yaani, The Civil Aviation (Aerial Work) Regulations na pia awe amepatiwa kibali kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga kwa kazi hiyo. Mmiliki wa ndege yeyote anayefanya shughuli za namna hii bila ya kuzingatia vigezo vya Kanuni hizi atachukuliwa hatua.
    5. Kutoa taarifa za matukio

      Rubani Mkuu ni lazima aandike taarifa ya matukio na kuiwasilisha Mamlaka ya Usafiri wa Anga kama ilivyoanishwa kwa mujibu wa kanuni za usafiri wa anga hususan, kanuni za 52, 74,75 na 76 zilizomo kwenye Kanuni ya The Civil Aviation (Operation of Aircraft) Regulations. Wananchi nao wanatakiwa kutoa taarifa ya tukio lolote waliloliona hatarishi kwa mujibu wa kanuni namba 262 ya Kanuni iliyotajwa.

      Mamlaka itafuatilia na kuchunguza taarifa inazozipokea na kuchukuwa hatua stahiki ili kuhakikisha kuwepo kwa usalama wa kiuendeshaji, watu na mali.
  4. HITIMISHO
    Ili kulinda usalama wa wananchi, wamiliki na marubani wote wanapaswa kuhakikisha wanazingatia Sheria ya Usafiri wa Anga pamoja na Kanuni zake. Rubani anayeendesha chombo ni lazima ahakikishe anatumia weledi wa hali ya juu katika matendo yake.

    Mamlaka inawahakikishia wananchi/umma kwa ujumla kwamba haitosita kuchukuwa hatua stahiki kama zilivyoanishwa kisheria na kanuni za usafiri wa anga iwapo mapungufu ya usalama yatajitokeza.
Imetolewa na
Charles M. Chacha
Kaimu MKURUGENZI MKUU
MAMLAKA YA USAFIRI WA ANGA TANZANIA

Ukweli Unauma: Jiwe walilolikataa CCM limekuwa jiwe kuu Chadema

By Padri Baptiste Mapunda
Injili inatufundisha kuwa enzi ya Yesu Kristo, baadhi ya watu walimwona ni kama kichaa na mvuruga amani katika jamii.

Wengine walimdharau hata kufikia hatua ya kusema “ huyu tunamjua, je, siyo mwana wa Yusufu na Mariamu?” Hata hivyo, Yesu aliendelea na kazi ya kuwaletea binadamu ukombozi.

Wakati viongozi wakuu, wasomi na maadui zake wakimtuhumu kwa utovu wa nidhamu, dhambi na mambo mengine, watu wa kawaida walizidi kumiminika na kumfuata.

Watanzania wa leo na hasa wanasiasa hawapendi kutumia maandiko matakatifu yanayopingana na matakwa yao au sera zao.Wanasiasa hupenda kutumia maandiko yale yanayotetea nafsi zao,masilahi yao na madaraka yao.

Mfano wa hili ni yale maandiko yasemayo: ‘’kila kiongozi anatoa mamlaka kwa Mungu kwa hivyo ni lazima kuyatii.” Lakini ukweli ni kwamba maneno ya Mungu ukiyatumia vibaya ni wazi lazima yatakuja kukugeuka muda si mrefu.

Kwa sababu maandiko matakatifu hasa Biblia ina majawabu yote yanayotafutwa na mwanadamu kwa sababu yanahusu historia ya mwanadamu na Mungu jinsi walivyotembea pamoja.

Ukitaka kujua kama unaendelea au la au upo sahihi katika mambo fulani ni lazima ulinganishe na mtu au kitu kingine au tukio fulani. Ukisikiliza hukumu za kesi mbalimbali utasikia hakimu ananukuu hukumu ya kesi iliyofanyika nchi fulani na hivyo kuifanya kama msingi wa hukumu anayoitoa. Wataalamu wanasema ‘hakuna jipya chini ya jua.’

Uchaguzi wa mwaka huu
Sasa tukirudi katika ulingo wa siasa za Tanzania na yanayotokea nyakati hizi hususani uchaguzi wa mwaka huu, tusifikiri ni tukio ambalo halijawahi kutokea popote duniani. La hasha! itakuwa ni kujidanganya. Siyo siri kwamba tangu waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa ahame CCM na kujiunga na Chadema, siasa za Tanzania zimebadilika, hili halina upinzani.

Sijui kama CCM walitabiri madhara ya kulikata jina lake mapema katika vikao vya juu vilivyofanyika kule Dodoma au na wao wanashangaa kama mimi.

Sasa hivi mazungumzo nchini Tanzania karibu kila kona ni Lowassa. Nilikwenda kuona wagonjwa hospitalini, nilikuta baadhi ya wagonjwa na mfanyakazi mmoja wakiwa katika mjadala mzito juu ya Mzee Lowassa. Mfanyakazi mmoja wa hospitalini hapo alitaka kupindisha ukweli, alipewa ukweli wake na wagonjwa waliokuwa karibu.

Walimwambia: “ Hatutaki kudanganywa kwani Lowassa kwa CCM kawa fisadi kwa vile ameondoka?” Hii ni alama wazi kwamba wananchi sasa wameanza kujitambua na kutambua kile kinachoendelea katika siasa zetu ikiwamo propaganda na porojo za kisiasa.

Ukweli ni kwamba kinachoonekana katika siasa za Tanzania kinalinganishwa na kilichotokea katika maisha ya Yesu. Alifanyiwa kila aina ya fitina, chuki, mizengwe hata akasalitiwa na rafiki yake Yuda na hatimaye akauawa kwa kutundikwa msalabani.

Kwa baadhi ya watu Yesu alionekana ni mzushi, alikuwa mchochezi katika jamii, alikuwa mvunja sheria za Wayahudi na mtu aliyekuwa anahatarisha amani ya jamii. Kuna mahali alifika akamponya mtu mwenye pepo kisha nguruwe wakaswagwa baharini.

Mzee Lowassa kajiondoa CCM na sasa amegeuka kuwa lulu na kivutio ndani ya Chadema, Ukawa na kwa Watanzania kwa jumla. Kwa mantiki hii kweli mzee Lowassa anaonekana kuwa kama jiwe lililokataliwa ndani ya CCM, lakini sasa limekuwa jiwe kuu ndani ya Ukawa.

Mzee Lowasa analaumiwa kuwa amekuwa akihonga ili watu wamuunge mkono katika harakati zake. Lakini kwa upande wangu ninashangaa kwani kadiri siku zinavyopita, watu wanaomuunga mkono wanaongezeka. Najiuliza hivi Lowassa ana fedha kiasi gani kuthubutu kuuhonga ule umati uliokusanyika Dar es Salaam, Mbeya, Arusha na hatimaye mjini Mwanza ?

Hakuna mtu au kiongozi aliyelaaniwa hapa duniani na kuchafuliwa, kutukanwa, kudharauliwa na kusiginwa kama Yesu mwana wa Yusufu, lakini hata hivyo watu kila siku alipokuwa anakwenda walikusanyika mamia kwa mamia kinyume cha matakwa ya maadui zake.

Najiuliza wale wote wanaomfuata Lowasa ni wehu, vichaa, wajinga na wapumbavu? Kufikiri hivi itakuwa ni makosa na kujidanganya, itakuwa ni kutafuta majibu mepesi kwa maswali magumu. Kuleta porojo katika jambo nzito kama hili ni kujiaibisha mbele ya umma.

Huku ni kumfanya Mzee Lowassa aonekane kama ‘ jiwe lililokataliwa ndani ya CCM na sasa limeguka kuwa jiwe kuu ndani ya Ukawa.”

Katika hatua hii ya Mzee Lowassa kukihama Chama cha Mapinduzi na kujiunga na chama kikuu cha upinzani nchini, anaonekana kuhama na baadhi ya vigogo wa CCM. Na sasa ukweli unaanza kujitokeza juu ya uhai, uimara, mpasuko, udhaifu na upungufu ndani ya chama hicho kikongwe barani Afrika.

Kwa mantiki hii utabiri wa Mwalimu Julius Nyerere juu ya upinzani wa kweli kutoka ndani ya CCM yenyewe, unaendelea kutimia siku hadi siku.

Kwa upande wangu, nazidi kupata nguvu ya kuandika kwamba ‘CCM imegeuka mnara wa Babel’.

Thursday 20 August 2015

Mheshimiwa Edward Lowassa asaini hati ya kiapo mahakama kuu ya kugombea Urais wa Tanzania

 Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa UKAWA kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mhe. Edward Lowassa akisaini fomu za hati ya kiapo kwenye ofisi za Jaji wa Mahakama ya Tanzania, Jijini Dar es salaam leo Agosti 19, 2015. Hati ambayo kila mgombea wa nafasi ya urais anatakiwa kusaini katika mahakama kuu jijini Dar es Salaam Kushoto ni Mgombea Mwenza, Juma Haji Duni.
 Mgombea mwenza wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa UKAWA kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt. Juma Haji Duni akisaini fomu za hati ya Kiapo kwenye ofisi za Jaji wa Mahakama ya Tanzania, Jijini Dar es salaam leo Agosti 19, 2015. Kushoto kwake ni Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa UKAWA kupitia Chama hicho, Mh. Edward Lowassa.
 Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa UKAWA kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mh. Edward Lowassa akipokea fomu za hati ya Kiapo kutoka kwa Jaji wa Mahakama ya Tanzania, Jaji Suleiman Said Komu.
 Mgombea mwenza wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa UKAWA kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt. Juma Haji Duni akipokea fomu za hati ya Kiapo kutoka kwa Jaji wa Mahakama ya Tanzania, Jaji Suleiman Said Komu. Kulia ni Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa UKAWA kupitia Chama hicho, Mh. Edward Lowassa.




Wednesday 19 August 2015

ORODHA YA MAJINA YA WANACHAMA WA CHADEMA WALIOTEULIWA KUGOMBEA UBUNGE

CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)
ORODHA YA MAJINA YA WANACHAMA WA CHADEMA WALIOTEULIWA KUGOMBEA UBUNGE