Lowassa ambaye ni waziri mkuu aliyejiuzulu Februari 2008, kuihifadhi Serikali ya CCM iliyokumbwa na kashfa ya mkataba wa Richmond, amechukua fomu hizo mchana leo akifuatana na viongozi wote wakuu wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Fomu hizo amezichukua kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CAHDEMA) ambacho kimepewa dhamana na UKAWA kuwakilisha umoja huo katika kampeni ya kukiondoa madarakani Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katika uchukuaji wa fomu, Lowassa alikuwa na mgombea wake mwenza, Juma Duni Haji, mwanasiasa gwiji aliyehamia Chadema akitoka Chama cha Wananchi (CUF) kwa lengo la kutimiza masharti ya UKAWA katika kusimamisha mgombea mmoja.
Duni alikuwa makamu mwenyekiti wa CUF, waziri wa Mawasiliano na Miundombinu na alishateuliwa kugombea kiti cha uwakilishi, jimbo la Bububu, mjini Zanzibar.
Viongozi waliofuatana na msafara wa Lowassa na Duni, ni wenyeviti wa vyama hivyo vinavyoshirikiana akiwemo Dk. Emmanuel Makaidi wa Chama cha National League for Democracy (NLD) na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.
Kiongozi mwingine ni James Mbatia, ambaye ni mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi. Wenyeviti wote hao ni wanatambuliwa kama wenyeviti wenza wa UKAWA.
Viongozi wengine ni makatibu wakuu wa vyama hivyo wakiongozwa na Maalim Seif Shariff Hamad wa CUF ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
MGOMBEA urais wa Tanzania kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambaye ni mwakilishi wa UKAWA, Edward Lowassa ameshtushwa kupokewa na umma mkubwa uliohudhuria wakati akichukua fomu za kugombea Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
“Haijawahi kutokea katika historia ya nchi yetu, maandamano makubwa kiasi hiki.
“Nimesimama kuwashukuru kwa jinsi mlivyojitokeza. Mmeandamana kwa heshima. CCM itaisoma namba mwaka huu,” alisema akitoa salamu kwa umma uliokusanyika kwenye uwanja wa Biafra, Kinondoni, Dar es Salaam.
“Muwahimize na wengine wajitokeze kupiga kura tarehe 25 Oktoba na ninawahakikishia tutashinda asubuhi siku hiyo,” alisema Lowassa aliyelazimika kufika eneo hilo ambako iliamuliwa sehemu ya wananchi wamsubiri kutokana na udogo wa eneo la makao makuu ya Chadema, mtaa wa Ufipa, Kinondoni.
Kutoka uwanjani Biafra alikopitia akitoka kuchukua fomu za urais makao makuu ya Tume, Lowassa aliongoza msafara pamoja na viongozi wakuu wa chama hicho pamoja na wale wa NCCR-Mageuzi, National League for Democracy (NLD) na Chama cha Wananchi (CUF), vinavyoshirikiana chini ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Lowassa ambaye alijiunga na Chadema mapema wiki iliyopita, ametoa salamu mahsusi kwa Jeshi la Polisi kwa kuongoza msafara kwa amani na utulivu mkubwa mpaka kukamilisha safari yake.
“Nawapongeza Jeshi la Polisi, leo wamekuwa waungwana. Tumewadhihirishia kuwa Chadema tunaweza kuongoza nchi,” amesema akirejelea hali ngumu iliyokuwepo Ofisi Kuu za CUF Buguruni ambako safari ilianzia.
Akihutubia umma hapo Kinondoni, mgombea mwenza, Juma Duni Haji alisema nia ya UKAWA ni kuongoza nchi ili kuwasaidia Watanzania kupata shibe na kuondokana na umasikini unaozidi kuumiza wananchi wanyonge.
Duni ambaye ametoka CUF na kuhamia Chadema kukamilisha utaratibu wa UKAWA kupata mgombea mwenza kutoka Zanzibar, alisema uongozi wa CCM umeshindwa kuondoa umasiniki, kwa sababu viongozi wake walikuwa wakihangaikia maslahi binafsi.
Umma ulikuwa mkubwa kiasi cha Polisi kupitia kwa Kamishna Suleiman Kova wa Kanda Maalum Dar es Salaam kutamka kuwa maandamano hayakuruhusiwa.
Msafara wa Lowassa ulipambwa na magari madogo, bajaji na pikipiki kutoka Buguruni mpaka msafara ulipowasili Kinondoni.
No comments:
Post a Comment